Rigathi Gachagua atengwa na baadhi ya wabunge wa Mt. Kenya

Wabunge wanapinga kauli y naibu wa rais ya mtu mmoja, shilingi moja na kura moja

Muhtasari

•Wabunge hao walijitenga na mwito wa Gachagua wa mtu mmoja, kura moja, shilingi moja

•Wabunge hao wanane kutoka kaunti ya Meru walijitenga na mwito wa Gachagua wa kutaka mtu mmoja, kura moja, shilingi moja

Rais William Ruto na Naibu wake Rigathi Gachagua
Image: ANDREW KASUKU

Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, amepata pigo kubwa baada ya baadhi ya viongozi kutoka Mlima Kenya kutokubaliana naye hadharani.

Katika taarifa ya Jumanne, Juni 4, wabunge hao wanane kutoka kaunti ya Meru walijitenga na mwito wa Gachagua wa kutaka mtu mmoja, kura moja, shilingi moja.

Wakati wa mkutano na wanahabari katika majengo ya Bunge, wabunge hao walisema kuwa wangejiepusha kuidhinisha mpango wa shilingi ya mtu mmoja unaoungwa mkono na viongozi wanaohusishwa na naibu rais Rigathi Gachagua.

Wabunge hao vilevile walitilia maanani msimamo wao thabiti wa Rais William Ruto dhidi ya migawanyiko ya kisiasa nchini.

Fauka ya hayo, wabunge hao waliunga mkono matamshi ya rais kwamba viongozi waliochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia, wanapaswa kujisikia huru kuzunguka nchi nzima mighairi ya kusumbuliwa.

Vilevile, walipinga msimamo wa Gachagua kwamba viongozi waliochaguliwa wanapaswa kushikamana na maeneo bunge yao na wala sio kuzurura kutoka eneo moja hadi jingine.

"Tunaunga mkono alichosema rais kuhusu hitaji la umoja tunapoendesha shughuli zetu nchini. Merus wako kila mahali. Sisi ni viongozi wa kitaifa. Tukihitajika popote tutaenda," Mwirigi alisema.

Wabunge wengine waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Rahim Dawood, Dorothy Ikiara, Mpuru Aburi, Julius Taituma, Dan Kili, na Moses Kirema.

Mgawanyiko na utengano wa wanasiasa umezidi kuibua maswali mengi kwani Rigathi Gachagua ni naibu wa rais ila kutokana na matamshi na cheche za matusi kutoka kwa viongozi wa Kenya Kwanza dhidi yake, wengi wanajiuliza iwapo serikali imetekeleza ahadi zake au wanaanzisha ugomvi wa kisiasa kabla hawajatimiza ahadi kwa wananchi.