Waandamanaji washangilia maafisa wa KDF wanaoshika doria na kuwasindikiza

Waandamani walipongeza maafisa wa KDF kwa kutowarushia gesi za kutoa machozi.

Muhtasari

• Waandamanaji hao pia wanasikika wakiimba nyimbo za kumpinga Rais William Ruto.

Magari ya KDF yakipitia mtaa wa Tom Mboya jijini Nairobi mnamo Juni 27, 2024. Picha: DAVICTOR MUNENE
Magari ya KDF yakipitia mtaa wa Tom Mboya jijini Nairobi mnamo Juni 27, 2024. Picha: DAVICTOR MUNENE
Image: DANVICTOR MUNENE

Waandamanaji jijini Nairobi siku ya Alhamisi walishangilia maafisa wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) walipokuwa wakiingia katikati mwa jiji la Nairobi.

Katika video maafisa wa KDF waliokuwa ndani ya magari yao walipitia barabara ya Tom Mboya ambapo walikutana na waandamanaji. Kisha wakaanza kuwashangilia huku wakiwasindikiza maafisa waliokuwa wakishika doria.

Waandamanaji hao pia wanasikika wakiimba nyimbo za kumpinga Rais William Ruto.

Maafisa hao wa KDF wamekuwa wakishika doria Jijini tangu Alhamisi asubuhi.

Kikosi kikubwa cha maafisa wa KDF kilionekana Alhamisi ndani ya uwanja wa Nyayo.

Pia kulikuwepo gari la kivita la KDF.

Maafisa hao wa KDF walionekana wakichukua maelezo kutoka kwa wakubwa wao kabla ya kutumwa.

Baadaye walionekana wakitoka Uwanjani wakielekea katika maeneo yao maalum ya kushika doria.

Wabunge siku ya Jumatano asubuhi waliidhinisha kutumwa kwa maafisa wa Jeshi la Ulinzi la Kenya ili kurejesha hali ya utulivu baada ya maandamano mabaya siku ya Jumanne.

Wanajeshi hao watapiga jeki maafisa wa polisi kurejesha hali ya kawaida kote nchini baada ya maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha kugeuka rabsha kali siku ya Jumanne.

Polisi siku ya Alhamisi walilazimika kuwatawanya baadhi ya waandamanaji waliokuwa tayari wamekusanyika katikati mwa jiji la Nairobi.

Waandamani walipongeza maafisa wa KDF kwa kutowarushia gesi za kutoa machozi.