Bangi ya thamani ya shilingi milioni 1.8 yanaswa Busia

Washukiwa wa ulanguzi watafutwa na polisi baada ya kukwepa vizuizi

Muhtasari

• Polisi wasaka washukiwa waliokuwa wakisafirisha misokoto ya bangi katika kaunti ya Busia Alhamisi.

• Bangi hiyo ilikuwa imewekwa katika magunia yenye nguo za mtumba za kuuzwa.

Magunia yenye misokoto ya bangi liyokamatwa na maafisa wa DCI Alhamisi 12, Septemba 2024 kaunti ya Busia.
Magunia yenye misokoto ya bangi liyokamatwa na maafisa wa DCI Alhamisi 12, Septemba 2024 kaunti ya Busia.
Image: image: DCI KENYA

Polisi na maafisa wa DCI kutoka kaunti ya Busia wanawasaka washukiwa wa ulanguzi wa mihadarati waliofaulu kukwepa mitego ya walinda usalama Alhamisi.

Washukiwa hao walitoroka na kuwacha bangi yenye thamani ya shilingi zilizokadiriwa kuwa milioni 1.8 kando ya barabara.

Bangi iliyokamatwa ilikuwa imewekwa katika misokoto 1,800 zenye urefu wa sentimita 45.

Taarifa ya DCI imesema kuwa walanguzi hao walikuwa wakisafiri kutumia pikipiki katika barabara ya Butula kuelekea Matungu. Walibadilisha mkondo na kutumia barabara ya Benga University waliposhusha mizigo hiyo haramu.

Misokoto ya bangi ilikuwa imefichwa katikati ya nguo za mtumba.

Takribani wiki moja iliyopita, polisi waliwakamata walanguzi wawili akiwemo mtoto wa miaka 17, wakisafirisha bangi yenye thamani ya shilingi milioni 1.32 yenye uzito wa kilo 44 katika barabara ya Nambale-Busia.

Juni mwaka huu tarehe 6, polisi wa Busia walipata magunia saba yenye uzani wa kilo 451 ya bangi yenye thamani ya shilingi milioni 13.