Jamaa aliyerekodiwa akisapoti mauaji ya wanawake atambuliwa, apigwa marufuku na klabu yake pendwa

Ronaldo na mwenzake walirekodiwa wakizungumza vibaya kuhusu wanawake na kuonekana kutetea mauaji ya wanawake.

Muhtasari

•Katika taarifa ya Jumamosi, Mathare Women FC ilikashifu kitendo cha ‘Ronaldo’ na kujitenga na matamshi yake mabaya

•Ijumaa, Ronaldo na mwenzake asiyejulikana walipokea shutuma nyingi kutoka kwa Wakenya baada ya video yao kusambaa.

amepigwa marufuku na Mathare Women FC
Ronaldo amepigwa marufuku na Mathare Women FC
Image: HISANI

Klabu ya soka ya Wanawake ya Mathare imempiga marufuku shabiki wao mmoja kwa jina la ‘Ronaldo’ kuhudhuria mechi zao.

Haya yanajiri baada ya video inayomuonyesha shabiki huyo na mwanamume mwingine asiyetambulika wakizungumza vibaya kuhusu wanawake na kuonekana kutetea mauaji ya wanawake yaliyokithiri nchini kusambaa kwenye mitandao ya kijamii. Wawili hao waliotatiza maandamano ya amani dhidi ya Mauaji ya Wanawake katika bustani ya Jevanjee siku ya Ijumaa walirekodiwa kwenye kamera wakiwakosoa wanawake na kutoa vitisho vya mauaji kwao.

Katika taarifa ya Jumamosi, Mathare Women FC ilikashifu kitendo cha ‘Ronaldo’ na kujitenga na matamshi yake mabaya.

Baada ya jana kuibuka kwa kanda ya video ya mmoja wa mashabiki wetu, Ronaldo, akitukana wanawake na kutoa maneno yasiyo na uwajibikaji yanayochochea ukatili dhidi ya wanawake, tumeamua kama timu kumfungia kabisa kuhudhuria mechi zetu, kuja kwenye viwanja vyetu au kujumuika na timu zetu kwa namna yoyote,” Mathare Women FC ilisema katika taarifa.

Taarifa hiyo ilisema zaidi, "Timu ya Mathare United Women haitawavumilia wahusika kama yeye, wanaoendeleza ukatili sio tu dhidi ya wanawake bali dhidi ya binadamu yeyote."

Waliambatanisha taarifa hiyo na picha ya Ronaldo akihudhuria moja ya mechi zao na kwenye picha hiyo waliandika “Marufuku.”

Ijumaa, Ronaldo na mwenzake asiyejulikana walipokea shutuma nyingi kutoka kwa Wakenya baada ya video yao kusambaa.

Mwanaharakati maarufu wa Kenya Boniface Mwangi alishiriki video hiyo kwenye akaunti yake ya Twitter na akatumia fursa hiyo kuwaomba wanaume wengine wajiunge katika maandamano ya kupinga mauaji ya wanawake.

Katika video hiyo, mwenzake Ronaldo alisikika akipinga maandamano ya amani ya wanawake wanaotetea kukomeshwa kwa visa vilivyokithiri vya mauaji ya wanawake.

Jamaa huyo alisikika akisema kuwa hata wanaume wameteseka sana mikononi mwa wanawake wanaodaiwa kuwapora pesa zao.

“Tutawaua! Tutawaua! Wengi iwezekanavyo," mwenzake Ronaldo alisikika akisema.

Ronaldo ambaye alikuwa amesimama karibu naye alisikika akimuunga mkono kwa kusisitiza kuwa watamaliza maisha ya wanawake.

“Hebu niwaambie, siwezi kukupeleka kwenye Pizza ukale pesa zangu.. C’mon, No way. Mtakufa! Mtakufa! Nyie wanawake mtakufa niwaambieni. Ati pesa unataka ya mwanaume. Mtakufa sana.” jamaa huyo aliongeza.

Waliendelea kusema kuwa visa vya hivi majuzi vya mauaji ya wanawake ni sehemu ndogo tu, na kutishia kuwa wanawake wengi zaidi watapoteza maisha yao.

Wawili hao wameendelea kukashifiwa sana na  Wakenya ambao wamekuwa wakitoa wito wa kukamatwa kwao