Mwanamke amchoma kisu mpenzi wake hadi kufa Nairobi

Mwanamke huyo alichukua kisu kutoka jikoni, akamchoma mpenziwe na kutoroka eneo hilo.

Muhtasari

•James Mungai Wirura alipatikana akiwa na maumivu ndani ya nyumba yake baada ya kudungwa kisu kifuani.

•Polisi walisema walipata silaha na nguo zilizolowa damu kama sehemu ya ushahidi.

Crime Scene
Image: HISANI

Mwanamke mmoja ameingia mitini baada ya kudaiwa kumdunga kisu na kumuua mpenzi wake katika mtaa wa Bahati, jijini Nairobi.

James Mungai Wirura alipatikana akiwa na maumivu ndani ya nyumba yake baada ya kudungwa kisu kifuani.

Alikimbizwa katika hospitali ambapo alitangazwa kufariki. 

Polisi na mashahidi wanasema marehemu aligombana na mpenzi wake aliyetambulika kwa jina la Everline kabla ya ugomvi huo kuwa vita.

Mwanamke huyo alichukua kisu kutoka jikoni, akamchoma mpenziwe na kutoroka eneo hilo.

Polisi walisema walipata silaha na nguo zilizolowa damu kama sehemu ya ushahidi.

Uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa marehemu alikuwa na majeraha mawili ya kisu kwenye kifua,karibu na moyo.

Mkuu wa polisi wa Nairobi James Mugera alisema wanachunguza tukio hilo na wanamsaka mshukiwa anayejulikana kujibu mashtaka kuhusiana na mauaji hayo.

Nia ya shambulio hilo la Jumamosi jioni bado haijajulikana.

Kwingineko huko Waithaka, polisi wanachunguza mauaji ya kijana wa umri wa miaka 25 ambaye mwili wake ulipatikana ukiwa kwenye dimbwi la damu.

Marehemu Ian Gichoya Mamui alipatikana na jeraha la kudungwa kisu kifuani.