Harambee Stars na Uganda Cranes wakabana koo

harambee stars
harambee stars
Harambee Stars na Uganda Cranes jana walicheza mechi ya kusisimua uwanjani Kasarani. Uganda walianza kufunga kunako dakika ya 22 kupitia kwa Emmanuel Okwi.

Francis Kimanzi alimuondoa Michael Kibwage baada ya muda wa mapumziko huku Johnstone Omurwa akichukua mahala pake. Kenneth Muguna alifunga bao la kusawazisha kunako dakika ya 51. Kimanzi alikisifu kikosi chake akisema amefurahishwa zaidi na wachezaji aliowaita.

Bingwa wa London Marathon Brigid Kosgei jana aliweka historia kwa kushinda taji la Great North Run huko Uingereza kwa kukimbia kwa saa moja 1 dakika 04 na sekunde 28. Kosgei alivunja rekodi ya awali ya mkenya mwenzake Mary Keitany aliyoweka mwaka 2014.

Muingereza Mo Farah alishinda taji la wanaume kwa mara ya sita mfululizo mbele ya muethiopia Tamirat Tola huku raia wa Uholanzi Abdi Nageeye, akimaliza katika nafasi ya tatu.

Henrikh Mkhitaryan alifunga mabao mawili na kusaidia mengine mawili Armenia walipiwanyuka Bosnia-Herzegovina mabao 4-2 katika mechi ya kufuzu kwa Euro 2020.

Kiungo huyo wa kati wa Arsenal ambaye anachezea Roma kwa mkopo alifunga bao la kwanza kunako dakika ya tatu. Alifunga la pili baada tu ya Edin Dzeko kusawazisha. Amer Gojak alisawazishia Bosnia tena lakini Hovhannes Hambard-zumyan akafunga kutokana na pasi ya Mkhitaryan.

Matokeo haya yanapiga jeki matumaini ya Armenia ya ubingwa wa Euro lakini yanawawacha Bosnia wakiwa mashakani. Armenia wako alama tatu nyuma ya Finland ambao wako katika nafasi ya pili.

Kwingineko, Juventus wanataka kufungua majadiliano ya mkataba na David de Gea mapema mwaka ujao iwapo mzozo wake na Manchester United hautakua umetatuliwa.

Raia huyo wa Uhispania atakua bila mkataba msimu ujao wa joto na hajatia saini mkataba wa pauni elfu 350 kwa wiki aliopewa na Manchester United.

Imeibuka kua wamiliki wa Juventus wanaweza kumtwaa De Gea bure bilash, na kumaanisha kua United watakosa kitita kikubwa cha ada ya uhamisho.