Hisia zaibuka baada ya Gor Mahia kutangazwa mabingwa wa KPL

Hisia mseto zimeibuliwa na baadhi ya wapenzi wa soka baada ya Mabingwa watetezi wa ligi kuu nchini, Gor Mahia kutawazwa mabingwa wa msimu wa mwaka  2019/2020.

Gor Mahia imelihifadhi taji hilo baada ya shirikisho la soka nchini FKF kutangaza kukamilika kwa msimu wa ligi kutokana na virusi vya Corona. Hata hivyo, baadhi ya wasimamizi wa KPL wamejitokeza na kupinga uamuzi huo wakisema kuwa haukufanywa kwa kuzingatia vigezo mbalimbali.

Hata hivyo, mwenyekiti wa shirikisho la soka nchini FKF Nick Mwendwa ameipongeza Gor Mahia kwa kushinda ligi huku akidokeza kwamba klabu ya City Stars vile vile imepandishwa daraja.

Real Madrid na Barcelona wamejiunga katika kinyang'anyiro cha kumsajili winga wa Borussia Dortmund na England Jadon Sancho.

Man United pia wako mbioni kumsaka nyota huyo mwenye umri wa miaka 20.

Vile Vile United inapigiwa upato kumnunua kiungo wa kati wa Aston Villa Jack Grealish mwenye umri wa  24, badala ya  mchezaji mwenza wa England na Leicester James Maddison aliye na umri wa miaka 23.

Licha ya Chelsea kuhusishwa na  nyota wa Brazil Philippe Coutinho, Barcelona imesema haitomuuza kiungo huyo matata  kwa bei ya chini ya pauni milioni 87. Mbali na hayo, Inter Milan wako tayari kubadilisha mkataba wa Victor Moses wa mkopo kuwa wa kudumu lakini wanaitaka Chelsea kusitisha mpango  wake wa  kumuuza winga huyo wa Nigeria aliye na miaka 29.