HONGERA! Malkia Strikers ndio mabingwa wa voliboli Afrika!

malkia strikers
malkia strikers
Malkia strikers walitoka nyuma na kuwanyuka Cameroon katika fainali ya voliboli ya kinadada kwenye mashindano ya All African games huko Rabat Morocco.

Kinadada hao wakiongozwa na kocha Paul Bitok walipoteza seti ya kwanza 12-25  kabla ya kurudi kwa kishindo na kushinda seti tatu za mwisho na kutetea taji lao.

Hayo yakijiri, Vanice Kerubo aliweka historia kwa kuwa mwanamke wa kwanza mkenya kushinda taji la bara la mbio za mita 400 kuruka viunzi kwa dakika 56.na sekunde 95.

Wakati huo huo Robert Kiprop, aliwaongoza Edward Zakayo na Richard Kimunyan kutwaa nafasi ya 1,2,3 katika mbio za wanaume za mita elfu 5.  Quailyne Jebiwott na George Manangoi pia walishinda mbio za mita elfu 1,500 kwa wanawake na wanaume mtawalia, huku Julius Yego akiongeza dhahabu nyingine ya javelin.

Kenya sasa inajivunia medali za dhahabu 11, za fedha 10 na kumi za shaba wakiwa katika nafasi ya 7. Misri Nigeria na Afrika Kusini zinaongeza jedwali zikufuatana.

Licha ya kukosa ufadhili, msimu wa KPL wa mwaka 2019/20 ulianza jana huku mechi mbili zikichezwa. Posta Rangers walitoka nyuma na kuwanyuka Sofapaka 2-1 na kupanda kileleni mwa jedwali wakiwa na alama 3.

Bao la Gerishon Likono kunako kipindi cha pili lilisawazisha la kutoka kwa Elly Asieche, kabla ya Eliud Lukwom la dakika ya 60 kuwapa ushindi. Wakati huo huo Kariobangi Sharks walitoka sare ya 2-2 na Western Stima.

Kocha wa Tusker Robert Matano anasema wako tayari kupambana na Gor Mahia katika mechi ya ufunguzi ya ligi kuu ya KPL, huku akiamini kuwa vijana wake ambao wamesajiliwa juzi watafanya vyema msimu huu.

Tusker walishinda ligi mara ya mwisho mwaka wa 2016 chini ya ukufunzi wa Matano na anaamini watashinda aitha ligi ama kombe la FKF msimu huu.

Timu ya Kenya wachezaji soka wa chini ya miaka 15 walinyukwa mabao 4-0 na Uganda katika fainali ya CECAFA kwa wachezaji wa umri huo huko Asmara Eritrea jana.

Mabao mawili ya Abasi Kyeyune na bao la Davis Ogwal na Travis Mutyaba yaliwapa ushindi Junior Cranes.