Kaunti nane zafuatiliwa kuhusu visa vya matamshi ya chuki - NCIC

Tume ya uiano na utangamano NCIC, inazifuatilia kaunti nane zinazorodheshwa kama maeneo yalio na visa vingi vya matamshi ya chuki.

Kaunti hizo ni Kiambu, Kilifi, Uasin Gishu, Elgeyo Marakwet, Baringo, Nakuru, Nyeri na Kakamega.

Afisa mkuu mtendaji wa tume hiyo Hassan Mohamed anasema wamezidisha vita dhidi ya matamshi ya chuki.

Haya yanajiri baada ya ongezeko la migawanyiko ya kisiasa ambayo imepelekea viongozi kutumia matamshi hayo kuwachochea wakenya. Ili kuthibiti matamshi ya chuki katika kaunti zilizotajwa, tume hio imeboresha mikakati ya kufuatilia matamshi hayo. Tume hio imetoa vinasa sauti, na kamera za kurekodi kwa maafisa wa usalama kutoka kwa kaunti hizo ili kuwarekodi wahusika.

 Tume hio pia inasema itahakikisha wanasiasa wanaohusishwa na matamshi ya chuki wanatozwa faini isiyozidi shilingi milioni moja au kifungo kisichozidi miaka mitatu gerezani au vyote viwili.

NCIC imesema katiba inatambua na kuunga mkono uhuru wa kujieleza, hata hivyo, uhuru huo hauruhusu uchochezi, matamshi ya chuki au propaganda za kuzua vurugu.

Wakenya kwenye mtandao wa Twitter kupitia kwa heshtegi # siku ya jumanne walidai kuchukuliwa hatua za haraka kumaliza matamshi ya chuki na wala sio vitisho tu.

Tume hio hata hivyo imesema sio matamshi yote yanayotolewa kwa misingi ya kikabila au rangi, ni ya chuki.