Kenya vs Tanzania: FKF huenda ikapigwa marufuku na FIFA

Shirikisho la soka nchini linahitaji shilingi milioni 19 ili kuandaa mechi ya marudio ya CHAN dhidi ya Tanzania jumapili ugani Kasarani. Shirikisho hilo linatathmini iwapo litawachia mechi hiyo na kukubali adhabu kutoka ikiwemo kupigwa marufuku, kutoka kwa FIFA.

FKF iliwasilisha bajeti hiyo kwa serikali lakini hawajapokea lolote. Kaimu afisa mkuu Barry Otieno anasema tayari wana madeni baada ya kuomba fedha za kuandaa mkondo wa kwanza uliochezwa Tanzania wiki iliyopita.

Kwingineko, timu ya kinadada ya voliboli nchini itaanza kampeni yao ya kufuzu kwa Olimpiki ya mabara kwa mechi dhidi ya Italia. Timu hiyo itakua bila Edith Wisa ambaye alishindwa kupata Visa kwa wakati ufaao baada ya kupoteza paspoti yake katika hali tatanishi.

Wisa sasa anasema ataangazia All Africa Games. Mechi inayofuata ya Malkia itakuwa dhidi ya Uholanzi kabla ya kukabana na Ubelgiji jumapili.

Kwenye raga, Kelvin Wambua anatarajiwa kuchukua uskani wa timu ya raga ya wachezaji saba baada ya KRU kutengana na Paul Murunga. Wambua ambaye alikua msaidizi wa Murunga msimu uliopita atasimamia timu hiyo kwa muda na atakua nao wakati wa michuano ya kufuzu kwa Olimpiki. Timu hiyo inatarajiwa kuregelea mazoezi baada ya Dala Sevens.