Nilivyofahamiana naye Prof Ken Walibora-Kennedy Wandera

Na Kennedy Wandera.

Nilikutana na Prof. Ken Walibora Juni 22, 2016 saa 8:02 katika makao makuu ya taasisi ya ukuzaji mitaala nchini Kenya KICD jijini Nairobi katika juhudi za kupanua na kueneza matumizi ya lugha ya Kiswahili ukanda wa Afrika Mashariki. Hapa palikuwapo wataalam na wanahabari wanaotumia Kiswahili. Hapa lengo lilikuwa moja tuKuzindua rasmi Chama cha Wanahabari wa Kiswahili Mashariki mwa Afrika-CHAWAKIMA. Lakini kwanza lengo letu lilikuwa ni kuanzisha Chama cha Wanahabari cha Kenya-CHAWAKIMA-KENYA kama tawi mojawapo la chama kikuu CHAWAKIMA.

Wadau wa Lugha waliohudhuria uasisi wa chama hiki walikuwa ni pamoja na Profesa Kenneth Inyani SimalaKatibu MtendajiKamisheni ya Kiswahili maarufu kama East Africa Swahili Commission, Profesa Ken WaliboraMwanahabariShirika la Habari la Nation, Charles OtungaMwanahabariShirika la Habari la KBC, Ramadhan KibugaMwanahabariShirika la Habari la BBC kutoka Burundi, Henry IndindiMtaalam wa Kiswahili, Jacob Riziki kutoka Burundi nami nikiwa Mwanahabari wa Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika, VOA. 

Dondoo za uzinduzi zilinakiwa na Bw Otungahapo kwenye kikao tukamteua Prof. Walibora kuwa Mwenyekiti nami naibu wake, Jacob Riziki aliteuliwa kuwa katibu kuendeleza mikakati ya kubuni chama cha wanahabari nchini Burundi-CHAWAKIMA-BURUNDI.

Mkutano huu ulifanyika baada ya kukamilika warsha ya siku mbili ya Baraza la Kiswahjili la Afrika mashariki lililozungumzuia kwa mapana swala zima la ustawishaji wa lugha ya Kiswahili na nafasi yake kwenye nyanja mbalimbali za maendelea hususan katika taasisi za elimu na maisha ya  wadau wa lugha hiyo.

Katika kikao hiki kilichoongozwa na Prof. Simalawanachama tulitakiwatukifuata itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya kuhamasisha umuhimu wa kubuniwa vyama vitakavyokuza lugha ya Kiswahili, Prof. Walibora alisisitizia umuhimu na jukumu la vyombo vya habari katika mchakato wa kukuza lugha ya Kiswahili kupitia mawanda mengine ya lughautafiti na uoanishaji wa mitaala na usanifishaji wa lugha katika nchi za Afrika Mashariki yaani Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi.

Katika mahojiano niliofanya naye ambayo yanapatikana hapa   kuanzia dakika ya 22:16-26:25. Prof. Walibora anaeleza hivi, “Vyombo vya habari vina wajibu mkubwa.Tunafikiria kuwa mustakabali wa Kiswahili ni mzuri sana lakini vyombo vya habari vina wajibu mkubwa wa kukisaidia kukieneza Kiswahili. Na kuundwa chama hiki ambacho sisi tunakiita CHAWAKIMA kitasaidia kusanifisha istilahi na msamiati unaotumika katika vyombo vya habari ili wasikilizaji wasitatanike sana.” 

Kutokana na juhudi hizo za Prof. Waliborachama hicho kipo hai kikiwa na wakilishi kutoka Zanzibar, Uganda, Kenya, Rwanda na Burundi. CHAWAKIMA-KENYA kimekuwa chini ya uongozi wake akiwa Msemaji wa chamaViongozi wengine wa chama hiki ni Mathias MomanyiMwanahabari na Mzalishaji wa vipindi KBC akiwa Mwenyekiti, Bw Otunga ni Mlezi wa chama, Victor Wetende ambaye ni mkurugenzi wa Mawasiliano katika serikali ya jimbo la Vihiga ni Katibu nami nikiwa Katibu Mwenezi huku Doreen Gatwiri akiwa Mwekahazina.

Prof. Walibora hakuwa tu msomi kama wasomi wengineAlisimama kidete na kazi za Kiswahili. Alifurahia wote waliokieneza kwa nguvu zao zoteNikimhoji Februari 23, 2017  kufuatia kifo cha mtunzi stadi wa mashairi Sheikh Ahmed Mohamed NabhanyMatondoni, Lamu nchini Kenya, Prof. Walibora alitumia maneno yote mazuri kumuomboleza Nabhany akimtaja kuwa mtu wa kupigiwa mfano katika uundaji wa misamiati na istilahi za lugha ya Kiswahili. Si wengi wanaopongeza tungo za wengineWalibora hakuwa na kiwi, hakuwa na kinyongoAlishabikia uwezo wa wandishi chipukizi na kwa wale walioonekana kujigamba na kujishabikia kuwa viranja wa lugha aliwakumbusha, “Kiswahili ni nyumba moja tusigombanie ufito

Oktoba 5, 2017 inasalia kwenye kumbukumbu, siku hii nilimtafuta Prof. Walibora kufahamu hisia zake kuhusu Tuzo ya fasihi ya Nobel inayotolewa na Taasisi ya Taaluma ya Uswidi kuhusu Lugha na Fasihi aliyopokezwa Kazuo Ishighuro,62, raia wa Uingereza. Msomi maarufu na mwandishi wa ‘Weep Not Child’, ‘A Grain of Wheat’ na ‘The River Between’ Professa Ngugi wa Thiong’o kwa mara ya pili alikuwa ameipoteza. Prof. Ngugi Wa Thiong’o tangu mwaka wa 2010 amekuwa akipigiwa upatu kushinda tuzo hii lakini bado hajabahatika. 

Profesa Walibora alionekana kutoshtuka na maamuzi ya jopo la Taasisi ya Taaluma ya Uswidi,  ‘Mimi sioni la ajabu wala sishangazwi na jopo linaloteua washindi wa tuzo ya Fasihi ya Nobel kutompa kwa mara nyingine Mkenya Ngugi wa Thiong’o. La msingi ni kwamba siku zote hata anapopigiwa upatu kwamba atashinda mimi huwa na shaka kwa sababu ya masuala ambayo labda hayaambatani moja kwa moja na ubora wa vitabu alivyoviandika au mchango wake katika uandishi wa fasihi barani Afrika au duniani kote hapana. La msingi ni kwamba tuzo ya fasihi ya Nobel hutolewa kwa mwandishi ambaye anaandika yale ambayo lile jopo linataka.”

Profesa Walibora hakujua kuficha uozo. Alieleza yaliokuwa moyoni bila kutetereka. Nimesema naye mwisho mwezi wa Machi mwaka huu kumhoji kupata ufafanuzi wake kuhusu mwelekeo wa kidiplomasia kati ya Kenya na Somalia. Wakati huu akifunza kwenye Chuo Kikuu cha Riara, Idara ya Diplomasia ya Kimataifa. Kabla ya hapo Februari 11, 2020 alinieleza jinsi alivyojaribu kunitumia fedha na badala yake zikamfikia kimakosa jamaa laghai, wakati akijaribu kumpigia simu hapokei. Harakati za kujaribu kufikia Safaricom kumrejeshea fedha hizo hazikufua dafu, zilikuwa tayari zimetumika. Kumsisitizia kuwa tuandikishe taarifa kwa polisi, Prof. Alinieleza “Wandera, uchumi wa Kenya umewabana wengi, watu wamekuwa wahuni, tusimlaumu.”

 Wengi wakiendelea kumuomboleza mwandishi wa riwaya ya ‘Siku Njema’, ‘Mbaya Wetu’, ‘Kidagaa Kimemwozea’, ‘Pepela na Mto’ ‘Ndoto ya Almasi’ miongoni mwa vitabu vinginemimi daima nitajivunia na kusherehekea muda niliotangamana naye.

  Kennedy Wandera, ni Mwandishi wa Habari, Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika, VOA, jijini Nairobi, Kenya.