Kupoteza pia ni kati ya mchezo,' Neymar apongeza Bayern kwa ushindi wao wa UEFA

Neymar ametumia mtandao wa kijamii kupongeza Bayern Munich baada ya miamba hao wa Ujerumani kubeba taji la Ligi ya Mabingwa.

Bayern, ambao wamekuwa na wakati mzuri kwenye kampeni yao, walinyuka kikosi cha Neymar, Paris Saint-Germain 1-0 mjini Lisbon mnamo Jumapili, Agosti 23 na kushinda taji hilo la Uropa.

Bao la Kingsley Coman dakika ya 59, kupitia kichwa liliweka mwanya kubwa kwenye mechi hiyo kali huku Bavarians wakinyakua ushindi.

Neymar, baada ya kusaidia PSG kuandikisha historia ya kuingia kwenye fainali ya kipute hicho alikuwa anapania kuongoza klabu hiyo ya Ufaransa kutwaa ushindi. Hata hivyo, Parisians walishindwa kutumia nafasi za mapema kufunga mabao na kupelekea kuadhibiwa na Bayern ambao walikuwa wamejinoa upande zote.

"Kupoteza pia ni kati ya mchezo, tunajaribu kila kitu na kupambana hadi mwisho,Asanteni kwa mchango wenyu na upendo wenyu mlionipa kila mmoja wenyu, na hongera kwa Bayern." Neymar Alizungumza.

Viongozi wa PSG walilazimika kumliwaza Neymar ambaye alibubujikwa na machozi baada ya kipenga cha mwisho kupulizwa. Lakini saa chache baadaye fowadi huyo alionekana kukubali matokeo na kutumia Twitter kupongeza Bayern.

Neymar pia aliwashukuru mashabiki kwa kusimama naye na kukiri kwamba kupoteza ni jambo la kawaida kwenye soka.