Maafisa 5 wa kaunti ya kiambu wakamatwa

Maafisa wa DCI wamewatia mbaroni wafanyikazi watano wa kaunti ya Kiambu kwa madai ya kutoa leseni bandia za matatu.

Watano hao akiwemo afisa wa uhasibu, afisa wa ICT, keshia wawili na afisa wa kushughulikia stakabadhi walikamatwa kufuatia ripoti kutoka kwa wananchi dhidi yao na kupelekea kufanyika kwa uchunguzi.

Elijah Mungai Mikinya, Lawrence Mutwiri Njebi, Mary Wairimu Nyota, Esther Njeri Waweru na George Njoroge Macharia walikamatwa siku ya Jumanne.

Tarakilishi kadhaa vikiwemo vipakatalishi zinazo shukukiwa kutumika kwa uhalifu huu zilinaswa kulingana na taarifa kutoka idara ya DCI kwenye twitter.

"Kutokana na madai ya kutolewa kwa leseni bandia za kaunti kwa wahudumu wa matatu katika eneo la kaunti ndogo ya Thika West maafisa wa @DCI Kenya walianzisha uchunguzi uliopelekea kukamatwa kwa washukiwa watano,” Mkurugenzi wa DCI George Kinoti alisema siku ya Jumanne.

Aliongeza kuwa ukaguzi zaidi utafanyiwa tarakilishi zote.