Man United wakalifisha Chelsea huku blues wakilalamikia VAR

VAR
VAR
Manchester United walipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Chelsea katika mechi ambayo vijana wa Frank Lampard walilalamikia kutotendewa haki baada ya uamuzi tata wa VAR dhidi yao.

United walikaribia alama tatu na Chelsea katika nafasi ya nne kupitia kwa mabao ya Anthony Martial na Harry Maguire katika kila kipindi ugani Stamford Bridge.

Chelsea walikasirika wakati Maguire aliepuka kadi nyekundu kwa kumpiga teke Michy Batshuayi kunako kipindi cha kwanza licha ya kisa hicho kuangaliwa na VAR.

Msururu wa habari za spoti;

Lewis Hamilton na Lionel Messi jana walituzwa kama wanaspoti wa mwaka katika hafla ya tuzo za Laureus jijini Berlin. Hii ni mara ya kwanza tuzo hili limepewa wanaspoti wawili.

Bingwa wa dunia katika mbio za marathon kwa wanaume Eliud Kipchoge alikuwa miongoni mwa wateuliwa wa tuzo hilo. Simone Biles mwana gymnast alishinda taji lake la tatu la Laureus la mwanaspoti bora wa kike. Washindi wa kombe la dunia la raga Afrika Kusini, walishinda tuzo la timu bora zaidi.

Pep Guardiola amewaambia wachezaji wa Manchester City kua amejitolea kusalia katika klabu hiyo, akisema hata kama wataishia katika League Two, bado atakuwepo. Raheem Sterling pia anasema atasalia City licha ya UEFA kuipiga marufuku ya miaka miwili kushiriki mechi za ubingwa bara ulaya, kwa kukiuka kanuni za utumizi wa fedha zilizowekwa, uamuzi ambao City itakataa rufaa dhidi, katika mahakama ya masuala ya spoti duniani.

Kumekuwa na tetesi tangu uamuzi huo kutolewa ijumaa kwamba huenda Guardiola akaondoka City.

Mkufunzi wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer haamini kuwa wakishindwa kujikatia tiketi ya kushiriki ligi ya mabingwa kutaathiri mpango wa uhamisho wa klabu hiyo. Wakati huo huo Solskjaer anasema uhamisho wa mkopo wa mshambuliaji wa Nigeria Odion Ighalo mwenye umri wa miaka 30, kuja Manchester United kutoka Shanghai Shenhua huenda ukafanywa wa kudumu.

Barcelona imekanusha madai kuwa iliajiri kampuni moja ya kuchapisha taarifa za kudhalilisha kwenye mitandao ya kijamii, zinazolenga wachezaji wake kama vile Lionel Messi na Gerard Pique.

Kituo kimoja cha redio kimedai kua Barcelona inataka kulinda hadhi ya rais wake Josep Maria Bartomeu na kuharibu ya wale ambao hawakubaliani naye.

Redio hio inadai kwamba klabu hio ilifanya kazi na kampuni ambayo huunda maoni katika akaunti za mitandao ya kijamii, ili kutekeleza hilo. Barcelona hata hivyo imejitenga vikali na akaunti hizo.