Afisa wa polisi anayetumia mbinu ya kipekee kukabili uhalifu Githurai

Tume ya huduma ya polisi kwa taifa hupendwa na wakati mwingine hukemewa kutokana na jinsi inavyoshughulikia ongezeko la uhalifu nchini.

Katika eneo la Githurai Nairobi tunapatana na Inspekta wa polisi Caroline Njuguna ambaye anasimamia kitengo cha makosa ya uhalifu katika kituo cha polisi eneo la Githurai.

Githurai ni eneo ambalo polisi wanasema kwamba kila siku kesi ya mauaji, uporaji wa mali, au kutekwa nyara kwa raia huripotiwa.

Licha ya kwamba eneo hilo linasemekana kuwa hatari sana kwa usalama kutokana na visa vingi vya uhalifu vinavyoripotiwa, Njuguna ameamua kutumia mbinu mpya kuukabili.

Kwa wakati moja alipatana na vijana wanaotumia dawa za kulevya na kujiingiza na visa vya uhalifu.

Hali ya vijana hao ilimgusa moyoni Njuguna na akaamua kuwatoa katika hali hiyo hatari.

Yeye anasema kituo chake kina askari wasiozidi 100, huku eneo hilo lina wakaazi zaidi ya 800,000. Hii huwa changamoto kubwa sana kudhibiti misururu ya kesi zinazoibuka kila siku.

Njuguna anajikita sana katika njia za kuzuia uhalifu badala ya adhabu.

"Kuwafungulia kesi wahalifu mahakamani si njia mwafaka ya kudhibiti, bali tunahitaji njia za kuwapa vijana wasio na kazi kitu mbadala cha kufanya wakiwa bila kazi," alisema.

Kwa sasa amewajumuisha maafisa wenzake katika kueneza kampeni inayojiita "Boots and Brains".

Lengo la kampeni hii ni kuhusisha jamii katika kuzuia uhalifu katika jamii na uraibu wa dawa za kulevya.

Tangu mwanzo mwa mwaka huu, Njuguna anasema wamezuru shule zote za umma katika eneo la Githurai na Kimbo na wanatazamia kuzuru shule zote eneo hilo.

Naibu OCPD wa Ruiru Edward Ndirangu anasema kwamba maafisa wanafurahishwa na juhudi zake ambazo zinaonekana kufaulu.