Barcelona yamfuta kazi Valverde na kumteua Setien

Getty Images
Getty Images

Barcelona imemtimua kocha Ernesto Valverde na badala yake kumteua kocha wa zamani wa Real Betis Quique Setien. Valverde, 55, aliisaidia kilabu hiyo kushinda mataji mawili mfululizo ya La Liga na wanaongoza kwa tofauti ya mabao msimu huu.

Walakini, timu hiyo ya Cataln imekuwa ikiandikisha msururu wa matokeo yasiyopendeza chini ya uongozi wake na walishindwa kufikia fainali ya ligi ya mabingwa bara Uropa.

Setien, 61, alisaidia Betis kumaliza katika nambari bora zaidi kwa mara ya kwanza kutoka mwaka wa 2005 na pia kuwawezesha kufika katika nusu fainali ya kombe la Copa del Rey kabla ya kuondoka mwezi Mei.

Amekubali kutia sahihi mkataba wa miaka miwili unusu na atawasilishwa kwa vyombo vya habari hii leo.

Hayo yakijiri,

Manchester United na Sporting Lisbon wamefanya mazungumzo ya ana kwa ana kuhusiana na uhamisho wa Bruno Fernandes kwa kitita cha pauni milioni 60. Kiungo wa kati Fernandes alifunga mabao mawili Sporting walipowanyuka Vitoria Setubal 3-1 Jumamosi. Raia huyo wa Ureno anataka uhamisho huo lakini hakujakuwa na makubaliano kati ya vilabu hivyo kuhusu ada.

Kiungo wa kati wa Ajax Donny van de Beek anatarajiwa kuondoka klabuni hiyo msimu huu wa joto na kutathmini uhamisho hadi kwa ligi ya Primia.

Mchezaji huyo wa miaka 22 amesema anatathmini uhamisho huo iwapo ofa itatolewa rasmi kufikia mwishoni mwa msimu huu. Wawakilishi wake wamekua katika mazungumzo na timu ya Uholanzi kuhusu nafasi bora kwake, lakini majadiliano hayajafanyika na Manchester United au klabu nyingine ya ligi ya Premier. Real Madrid wanataka kumsajili lakini hakuna makubaliano yalioafikiwa.

AC Milan wanatayarisha ofa ya pauni milioni 15 kwa kiungo wa Tottenham Hotspur Serge Aurier. Mwenyekiti wa Spurs Daniel Levy anakisiwa kuwa huenda akaikataa ofa hiyo na kuiambia klabu hiyo ya Italia kuongeza kitita kabla ya makataa ya uhamisho wa mwezi Januari.