Mark Otieno aomba kuondolewa marufuku yake baada ya maabara kuthibitisha hakutumia dawa za kusisimua misuli

Muhtasari

•Otieno anataka marufuku iliyowekwa dhidi mwaka jana kuondolewa baada matokeo ya maabara kubaini kuwa hakutumia dawa za kusisimua misuli.

•Mwanariadha huyo ameeleza kwamba amekuwa akipitia kipindi kigumu katika juhudi za kusafisha jina lake na kuthibitisha kuwa hana hatia.

Bingwa wa mbio za mita 100 Mark Otieno Odhiambo ameomba kuruhusiwa kushiriki tena katika mashindano.

Otieno anataka marufuku iliyowekwa dhidi mwaka jana kuondolewa baada matokeo ya maabara kubaini kuwa hakutumia dawa za kusisimua misuli.

Kupitia taarifa, Mwanariadha huyo amesema kuwa matokeo ya maabara ambayo alipokea miezi kadhaa iliyopita yaliashiria kuwa kirutubisho alichokuwa akitumia kilikuwa kimechafuliwa kwa dawa isiyotajwa ambayo imepigwa marufuku.

"Miezi kadhaa iliyopita nilipokea matokeo kutoka kwa maabara iliyopitishwa na WADA yakithibitisha mashaka yangu kwamba mojawapo ya virutubisho vya lishe ambavyo nilikuwa natumia vilichafuliwa kwa kitu kilichopigwa marufuku ambacho kilisababisha kipimo + kwenye Olimpiki za Tokyo. Matokeo haya yanathibitisha bila shaka kwamba sikutumia madawa ya kusisimua misuli kama ambavyo nimekuwa nikisisitiza tangu mwanzo," Otieno amesema.

Mwanariadha huyo ameeleza kwamba amekuwa akipitia kipindi kigumu katika juhudi za kusafisha jina lake na kuthibitisha kuwa hana hatia.

Amesema kuwa tayari ameandika barua kwa wahusika wote akiomba marufuku aliyowekewa iondolewe ili aruhusiwe kukimbia tena.