Wanariadha wa Afrika wajipata katika uchunguzi wa mbio za nusu marathon za China

Wanariadha wa Kenya na Ethiopia wachunguzwa kwa madai ya kupanga matokeo ya mbio za nusu marathon za China.

Muhtasari

• Waafrika watatu walionekana kupunguza kasi walipokaribia mstari wa kumalizia na kuashiria mara kwa mara He awafikie hadi kwenye utepe wa kumalizia .

Waandalizi wa mbio za Beijing Half Marathon wameanzisha uchunguzi kuhusu madai ya upangaji wa matokeo ya mbio zinazohusisha wanariadha wa Ethiopia na Kenya.

Katika picha ambazo zimesambaa kwenye mitandao ya kijamii, mwanariadha wa Ethiopia Dejene Hailu na wanariadha wa Kenya Robert Keter na Willy Mnangat walionekana kumwachia kimakusudi mwanariadha wa China He Jie kushinda mbio za nusu marathon siku ya Jumapili.

Waafrika watatu walionekana kupunguza kasi walipokaribia mstari wa kumalizia na kuashiria mara kwa mara He awafikie hadi kwenye utepe wa kumalizia .

He, mshindi wa medali ya dhahabu ya mbio za marathon za Michezo ya Asia 2023, kisha alipongezwa na wanariadha watatu wa Kiafrika baada ya kushinda mbio hizo kwa sekunde.

Baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wa Uchina wamekosoa ushindi wake kuwa "wa aibu" na usio wa kiuanamichezo, huku kukiwa na uvumi kwamba matokeo ya kinyang'anyiro hicho yalichakachuliwa.

"Tunachunguza na tutatangaza matokeo kwa umma mara tu yatakapopatikana," mwakilishi wa Ofisi ya Michezo ya Beijing aliambia shirika la habari la AFP siku ya Jumatatu.

Mratibu wa mbio za marathon pia alithibitisha kuwa uchunguzi umeanzishwa, AFP iliripoti.

He, Hailu, Keter au Mnangat hawajatoa maoni yao kuhusu uchunguzi huo.