MP Barasa: Kenya Kwanza kutawala kwa miaka 50

Mbunge huyo wa UDA alisema Kenya Kwanza itatawala kwa angalau miaka 50 hata bila kuondoa ukomo wa muhula wa urais.

Muhtasari

• Barasa alisema kuwa mwendelezo wa serikali ya Kenya Kwanza utaafikiwa kwa kuhakikisha kuwa mrithi wa Rais William Ruto atakuwa kutoka muungano unaotawala.

Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa
Image: MAKTABA

Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa amejitosa kwenye mjadala mkali kuhusu shinikizo la kuondoa kikomo cha mihula ya urais.

Mbunge huyo wa UDA alisema Kenya Kwanza itatawala kwa angalau miaka 50 hata bila kuondoa ukomo wa muhula wa urais.

Barasa alitofautiana na viongozi wanaoshinikiza kuondolewa kwa ukomo wa muhula wa kikatiba akisisitiza kuwa hata bila hivyo, muungano unaotawala unaweza kutawala kwa angalau nusu karne.

"Jambo pekee ambalo tungetaka kuendelea ni kwamba tungetaka serikali ya Kenya Kwanza itawale angalau kwa miaka 50 ijayo," Barasa alisema katika mahojiano ya asubuhi kwenye runinga ya K24.

Mbunge huyo alieleza kuwa msimamo wake kwamba Kenya Kwanza itatawala kwa angalau miaka 50 haimaanishi kuwa muhula wa urais wa miaka 10 utafutiliwa mbali.

"Tunaweza kufanya hivyo na kufikia lengo hilo kwa kutoondoa kikomo cha muda," alisema.

Barasa alisema kuwa mwendelezo wa serikali ya Kenya Kwanza utaafikiwa kwa kuhakikisha kuwa mrithi wa Rais William Ruto atakuwa kutoka muungano unaotawala.

“Tutahakikisha kwamba pindi tu Rais Ruto atakapokamilisha hatamu yake ya miaka 10 kikatiba basi yeyote atakayekuja ataichukua kutoka kwa maendeleo ambayo William Ruto atakuwa amefanya wakati huo,’’ akasema.

Barasa alisema Kenya Kwanza itakuwa katika ligi moja na Chama Cha Mapinduzi cha Tanzania na ANC ya Afrika Kusini kwa kuhakikisha inaendelea hata baada ya Ruto kuondoka.

Vyama hivyo viwili ni baadhi ya vyama ambavyo vimetawala kwa miongo kadhaa barani Afrika, muda mrefu baada ya waasisi wao kuondoka madarakani.

Mbunge huyo alikuwa akichangia mjadala wa shinikizo la kuondoa ukomo wa mihula ya urais ili kumruhusu Rais Ruto kutawala milele.

Mbunge wa Pokot Kusini, David Pkosing, wiki jana alizua mjadala kuhusu suala hilo baada ya kusema kulikuwa na mpango wa kuondoa ukomo wa muhula wa urais. Alizungumza huko Pokot Magharibi wakati wa hafla ya kuzindua kiwanda cha kutengeneza saruji iliyohudhuriwa na Rais. 

Wakati wa hafla hiyo, Mwenyekiti wa Devki, Narendra Raval aliambia hadhira kwamba Rais Ruto anafaa kutawala Kenya kwa angalau miaka 25, akiomba kwamba Mungu ampe miaka 100 ya maisha. “Rais wetu yuko hapa na nina furaha. Nilikuwa na wasiwasi kuhusu hali ya hewa lakini alijitahidi sana na kuja hapa hata na magari. Anatupenda sana. Anaipenda nchi hii sana- haswa mimi mwenyewe, sina maneno ya kumwambia. Mungu akupe miaka 100 ya maisha. Natamani tungekuwa na Rais huyu kwa angalau miaka 25… Ataibadilisha nchi hii. Sitaki kusema mengi, sitaki kuchukua muda wake mwingi kwa sababu ana majukumu mengine mengi,” alisema Raval.