Mwanariadha Faith Chepkoech mwenye umri wa miaka 21 amepigwa marufuku kushiriki mbio zozote baada ya kupatikana na hatia ya kutumia dawa za kusisimua misuli na shirika linalodhibiti utumizi wa dawa hizo.
Katika taarifa ambayo ilitolewa na shirika hilo, Chepkoech alipatikana na hatia hiyo baada ya vipimo ambavyo vilifanyika tarehe 26 Julai,vilionyesha kuwa kinda huyo alikuwa ametumia dawa dawa aina ya EPO.
Vipimo hivyo vilichukuliwa mnamo tarehe 4 septemba maeneo ya Iten,Elgeyo-Marakwet kutoka kwa sampuli ya mkojo kutoka kwa mwanariadha huyo na kufanyiwa vipimo kwenye maabara kuu ya shirika hilo mjini Cologne,Ujerumani.
Baada ya kupatikana kwa EPO ambayo adhabu yake ni marufuku ya miaka minne, Chepkoech alipewa kipunguzio cha mwaka mmoja baada ya kukubali kosa lake na ambalo linavunja kanuni ya 10.8.1 ya kanuni za utumizi wa dawa za kusisimua misuli.
Licha ya Chepkoech kuwa na matumaini usoni kwenye tasnia ya riadha, kwa maana atakuwa na umri wa miaka 24, wakati marufuku yake itaisha. Kutokana na marufuku hiyo Chepkoech ataupoteza ushindi wake wa riadha za pre-classic za mita elfu kumi kwa mda wa 30:22.77 ambapo alishinda kima cha $10,000.
Kufuatia kusikizwa kwa kosa lake,alipatikana kuwa hakuwa na sababu tosha za kutumia dawa hiyo na kwa hivyo kuangukiwa na shoka la marufuku ya miaka mitatu.