Matokeo ya wiki ya tatu ya EPL 2021/22 na jinsi jedwali ilivyo kwa sasa

Kwa sasa Tottenham inashikilia nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 9 huku Westham, Manchester United na Chelsea zikifunga nne bora na pointi 7 kila mmoja.

Muhtasari

•Mechi tano zilichezwa mida ya saa kumi na moja jioni ya Jumamosi.

•Mechi tatu zilipigwa siku ya Jumapili za kwanza zikiwa kati ya Burnley na Leeds na Tottenham dhidi ya Watford ambazo zilichezwa mida ya saa kumi alasiri.

Mason Greenwood akisherehekea bao lake dhidi ya Wolves siku ya Jumapili
Mason Greenwood akisherehekea bao lake dhidi ya Wolves siku ya Jumapili
Image: TWITTER

Wiki ya tatu ya msimu wa EPL 2021/22 imetamatika huku mechi kumi za kusisimua zikipigwa wikendi ambayo imepita.

Mechi ya kufungua wiki ya tatu ilkuwa kati ya mabingwa Manchester City na vigogo wa Arsenali ambapo Wanabunduki walionyeshwa kivumbi kikubwa ugani Etihad mida ya saa nane unusu alasiri ya Jumamosi.

Ikay Gundogan, Ferran Torres , Gabriel Jesus na Rodri walisaidia vijana wa Pep Guardiola kupata ushindi mkubwa wa 5-0 na kuwafikishia pointi 6 huku vijana wa Mikel Arteta wakiwa bado hawajaandikisha pointi  wala bao lolote msimu huu.

Mechi tano zilichezwa mida ya saa kumi na moja jioni ya Jumamosi.

Leicester walilaza Norwich mabao mawili kwa moja ugani Carrow Road ulioko jijini Norwich, Everton wakanyuka Brighton ugenini mabao mawili kwa nunge kupitia mshambulizi Dominic Calvert-Lewin na Demarai Gray.

Mechi kati ya Aston Villa na Brentford, Newcastle na Southampton na Westham na Crystal Palace ziliishia sare ya 1-1, 2-2 na 2-2 mtawalia.

Mchuano wa kufunga siku ya Jumamosi ulikuwa kati ya miamba wawili wa soka bara Ulaya Liverpool na Chelsea. Mshambulizi Kai Havertz alifungia Chelsea bao maridadi katika dakika ya 22 ila kadi nyekundu iliyopatiwa mlinzi Recce James na penalti iliyofungwa na mshambulizi wa Liverpool Mohammed Salah kufuatia kosa la James lilikatiza ndoto za Chelsea kuendelea kukaa kileleni mwa jedwali la EPL  huku timu hizo mbili zikigawana pointi ugani Anfield.

Mechi tatu zilipigwa siku ya Jumapili za kwanza zikiwa kati ya Burnley na Leeds na Tottenham dhidi ya Watford ambazo zilichezwa mida ya saa kumi alasiri.

Burnley na Leeds zililazimika kugawana pointi baada ya mechi hiyo kuisha sare  ya 1-1.

Tottenham ilipanda hadi kileleni mwa jedwali la EPL baada ya kuadhibu Watford bao 1-0 wakiwa nyumbani. Bao la pekee la mshambulizi Son Heung-Min lilisaidia vijana wa Nuno Espirito Santo kupata ushindi huo muhimu

Mechi ya mwisho katika wiki ya tatu ilikuwa mechi ngumu kati ya Wolves dhidi ya miamba wa Manchester United. 

Bao la kijana Mason Greenwood katika dakika ya 80 lilisaidia Mashetani Wekundu kupata ushindi wa 0-1 ugenini na kuwawezesha kufikisha pointi saba.

Kwa sasa Tottenham inashikilia nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 9 huku Westham, Manchester United na Chelsea zikifunga nne bora na pointi 7 kila mmoja.

Masaibu yanaendelea kuandama wanabunduki huku sasa wakishikilia nafasi ya mwisho bila pointi wa bao lolote. Wolves na Norwich pia hawajaweza kuandikisha pointi yeyote.