Manchester United yawaaga kwaheri Pogba na Lingard

Muhtasari

•United tayari imewaaga kwaheri wawili hao huku mikataba yao ikitarajiwa kuisha mwishoni mwa mwezi huu wa Juni.

•Katika taarifa ambayo ilitolewa Jumatano, United iliwatakia Pogba na Lingard kheri njema katika hatua yao ifuatayo.

Image: HISSANI// MANCHESTER UNITED

Klabu ya Manchester United imetangaza kuwa wachezaji wake wawili, Paul Pogba and Jesse Lingard watakuwa wanaondoka.

United tayari imewaaga kwaheri wawili hao huku mikataba yao ikitarajiwa kuisha mwishoni mwa mwezi huu wa Juni.

Lingard ambaye alijiunga na Mashetani Wekundu katika kiwango cha Under-9s atakuwa anaondoka baada ya kuchezea klabu hiyo kwa takriban miongo miwili.

Raia huyo wa Uingereza alianza kuchezea timu ya kwanza ya united mwaka wa 2014 na ameshiriki katika mechi 232 kufikia kuondoka kwake.

Pogba ambaye alijiunga na United akiwa na umri wa miaka 16 baada ya kushiriki katika mechi 233 za klabu hiyo.

Kiungo huyo wa kati alikuwa ameondoka  United mwaka wa 2012 na kujiunga na Juventus ila akarejea tena mwaka wa 2016. 

Katika taarifa ambayo ilitolewa Jumatano, United iliwatakia Pogba na Lingard kheri njema katika hatua yao ifuatayo.

Hata hivyo mipango ya wawili hao kuelekea msimu ujao bado haijabainika wazi huku tetesi kadhaa tu zikichimbuka.

Huku mkataba wao na United ukiwa unaelekea kutamatika inamaanisha kuwa wawili hao sasa ni wachezaji huru.