Rasmi! Antonio Rudiger ajiunga na Real Madrid kutoka Chelsea

Muhtasari

•The Blues walimuaga kwaheri Rudiger siku ya Alhamisi baada ya kuwa nao kwa kipindi cha miaka mitano.

•Rudiger amesema kwamba yupo tayari kwa changamoto mpya  nchini Uhispania akiwa na klabu yake mpya ya Madrid.

Antonio Rudiger (29)
Antonio Rudiger (29)
Image: CHELSEA.COM

Beki matata kutoka Ujerumani Antonio Rudiger amekamilisha uhamisho wake kutoka Chelsea hadi Real Madrid.

The Blues walimuaga kwaheri Rudiger siku ya Alhamisi baada ya kuwa nao kwa kipindi cha miaka mitano.

Rudiger ,29, anajiunga na Real Madrid bila ada yoyote kwani mkataba wake na Chelsea unaelekea kuisha.

"Beki huyo wa Ujerumani ameondoka The Blues na kujiunga na Real Madrid, akiwa ametoa mchango mkubwa katika mafanikio yetu katika misimu ya hivi karibuni. Rudiger alinyanyua Kombe la FA, Ligi ya Mabingwa, Ligi ya Europa, UEFA Super Cup na Kombe la Dunia la Vilabu la FIFA akiwa na Chelsea huku akicheza jukumu muhimu katika ushindi huo wote katika moyo wa ulinzi wetu,"  Chelsea ilitangaza kupitia taarifa.

Beki huyo ambaye alijiunga na Chelsea mwaka wa 2017 anaondoka baada ya kuwakilisha klabu hiyo katika mechi 203 na kuifungia jumla ya mabao 12. The Blues wamesema Rudiger hakuwa mchezaji mahiri tu bali pia kiongozi shupavu kwa timu hiyo.

Rudiger amesema kwamba yupo tayari kwa changamoto mpya  nchini Uhispania akiwa na klabu yake mpya ya Madrid.

"Ninajivunia kutangaza kuwa nitakuwa najiunga na Real Madrid. Nina furaha kubwa kwa changamoto zilizo mbele  na siwezi kusubiri kucheza mechi zangu za kwanza kwa klabu hii kubwa," Rudiger alisema kupitia Twitter.

Real ilimkaribisha beki huyo kupitia kurasa rasmi za mitandao ya kijamii na kutangaza kuwa atazinduliwa rasmi kama mchezaji wao mnamo Juni 20.

"Tumeimarisha kikosi chetu kwa kumsajili mmoja wa mabeki bora katika soka la dunia baada ya mchezaji huyo wa kimataifa wa Ujerumani kujiunga na klabu hiyo akitokea Chelsea. Alikuwa kiungo muhimu wa timu hiyo ya London iliyonyanyua Ligi ya Mabingwa, Ligi ya Europa, Kombe la Dunia la Klabu, UEFA Super Cup na Kombe la FA. Pia ameshiriki katika Timu bora ya Ligi ya Mabingwa katika misimu miwili iliyopita," Real ilitangaza.

Rudiger anatazamiwa kushiriki mechi zake za kwanza na Real katika msimu wa 2022/23 ambao utangoa nanga mwezi Agosti.