PSG yamfuta kazi kocha Mauricio Pochettino baada ya miezi 18!

Muajentina huyo aliingia PSG miezi 18 iliyopita akitokea Tottenham Hotspurs.

Muhtasari

• Inadaiwa Pochettino alifutwa kazi baada ya kushindwa kuisaidia timu kutwaa ubingwa wa bara Uropa.

Kocha Mauricio Pochettino
Gatty Images Kocha Mauricio Pochettino
Image: BBC Sport

Klabu cha soka cha PSG kutokea Ufaransa wametangaza kuvunja mikataba yake ya kikazi na kocha mkuu wa timu hiyo, Muajentina Mauricio Pochettino.

Katika taarifa kwa umma ambayo iliwekwa wazi Jumanne alasiri, PSG wamekiotesha kibarua cha Pochettino nyasi baada ya kocha huyo kudumu klabuni humo kwa miezi 18.

Pchettino alitwaa mikoba ya ukufunzi katika klabu ya PSG akitokea Tottenham Hotspurs ya Uingereza alikodumu kwa miaka mingi kama kocha na kuiletea timu hiyo mafanikio makubwa, kubwa likiwemo kuwafikisha katika fainali ya klabu bingwa barani Uropa, mwaka 2019.

Alifutwa kazi msimu uliofuatia baada ya matokeo ya kutoridhisha ambapo nafasi yake ilitwaliwa na Mreno Jose Mourinho.

Pochettino anaiaga PSG baada ya kushindwa kuwasaidia miamba hao wa Ufaransa kulitwaa taji la Champions League ambalo wamekuwa wakilimezea mate kwa muda mrefu bila ya mafanikio.

Msimu jana, klabu hiyo inayomilikiwa na bilionea kutoka miliki za Kiarabu iliandikisha historia baada ya kumnunua mshambuliaji nguli Lionel Messi kutoka Barcelona kwa lengo la kuimarisha matumaini yao ya kushinda Champions League lakini bado walibanduliwa nje ya kampeni za taji hilo katika hatua ya 16 bora.

Tayari PSG ishapata mrithi wa Pochettino ambapo muda mfupi baada ya kufutwa kazi, klabu hiyo ilitangaza nafasi hiyo kuzibwa na kocha Christopher Galtier akitokea klabu ya Nice ambacho pia kinashiriki katika ligi kuu ya Ufaransa, Ligi 1.