Bingwa tena! Julius Yego anyakua shaba kwenye mashindano ya Jumuiya ya Madola

Yego pia alifanikiwa kuandikisha matokeo yake bora katika kipindi cha miaka mitatu.

Muhtasari

•Yego alitwaa medali hiyo baada ya kutupa mkuki umbali wa mita 85.70 katika fainali za mashindano ya Jumuiya ya Madola.

•Wyclife Kinyamal alishindia Kenya nishani ya dhahabu katika mbio za mita 800 baada ya kukimbia kwa dakika 1.47.52.

•Beatrice Chebet pia aliongeza dhahabu kwenye kabati ya medali za Kenya baada ya kuibuka mshindi katika mbio za mita 5000. 

Julius Yego alishinda shaba kwenye mashindano ya Commonwealth mnamo Agosti 7, 2022
Julius Yego alishinda shaba kwenye mashindano ya Commonwealth mnamo Agosti 7, 2022
Image: HISANI

Bingwa wa kurusha mkuki wa Kenya Julius Yego almaarufu Youtube man amerejea katika ukumbi wa ushindi baada ya kunyakua shaba kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola inayoendelea Birmingham, Uingereza.

Yego alitwaa medali hiyo baada ya kutupa mkuki umbali wa mita 85.70 katika fainali za mashindano hayo zilizofanyika usiku wa kuamkia Jumatatu.

Arshad Nadeem wa Pakistani alivunja rekodi ya taifa lake na kunyakua dhahabu baada ya kutupa mkuki kwa umbali wa mita 90.18. Anderson Peters wa Grenada naye alitwaa fedha kwenye mashindano hayo kwa kutupa umbali wa mita 88.64.

Kando na kushinda nishani, Yego pia aliandikisha matokeo yake bora katika kipindi cha miaka mitatu.

Miaka ya hivi majuzi, bingwa huyo wa dunia mwaka wa 2015 amekuwa akipambana na majeraha ambayo yametatiza azma yake ya kuendelea kung'aa.

Mara ya mwisho kwa Yego kutupa mkuki umbali wa zaidi ya mita 85  ilikuwa kwenye michezo ya Afrika iliyofanyika Morocco mwaka wa 2019 ambapo alitupa umbali wa mita 87.73 na kunyakua dhahabu.

Wakati huohuo, Wyclife Kinyamal alishindia Kenya nishani ya dhahabu katika mbio za mita 800 baada ya kukimbia kwa dakika 1.47.52.

Beatrice Chebet pia aliongeza dhahabu kwenye kabati ya medali za Kenya baada ya kuibuka mshindi katika mbio za mita 5000. 

Sellah Busienei aliweza kunyakua shaba katika mbio hizo za miita 5000M upande wa wanawake zilizofanyika Jumapili usiku.