Kakake Paul Pogba, Mathias ashtakiwa kwa 'unyanganyi' wa fedha za nduguye

Watu wengine wanne pia wanachunguzwa rasmi kwa ulaghai na uhalifu huo.

kumuunga mkono kwenye sherehe za ubingwa wa kombe la dunia walioupata timu ya taifa ya Ufaransa mwaka 2018
Mathias (kulia) akiwa na ndugu yake Pogba kumuunga mkono kwenye sherehe za ubingwa wa kombe la dunia walioupata timu ya taifa ya Ufaransa mwaka 2018
Image: BBC

Mathias Pogba amefunguliwa mashtaka na kuwekwa kizuizini kwa madai ya kula njama ya unyang'anyi ama kutaka 'kumuibia' pesa kwa mabavu, kaka yake Paul, ambaye ni kiungo wa kati wa Ufaransa na Juventus.

Watu wengine wanne pia wanachunguzwa rasmi kwa ulaghai na uhalifu huo, vyanzo vya mahakama viliambia mashirika ya habari ya Reuters na Agence France-Presse.

Wakili wa Mathias Pogba, Yassine Bouzrou, alisema mteja wake hana hatia. Aliliambia shirika la utangazaji la Ufaransa BFMTV: "Tutapinga uamuzi huu."

Mathias Pogba, 32, amekiri kuwa anahusika na video ambayo ilionekana mtandaoni mwezi uliopita ikiahidi "kufichua" mambo kadhaa yanayomuhusu kiungo huyo wa kati wa Juventus mwenye umri wa miaka 29.

Waendesha mashtaka wa Ufaransa walifungua jalada la uchunguzi wa kimahakama mapema mwezi huu baada ya mchezaji wa zamani wa Manchester United Paul kusema alikuwa analengwa na unyang'anyi na vitisho kutoka kwa genge moja la uhalifu linalomuhusisha ndugu yake.

Aliwasilisha malalamiko yake kwa waendesha mashitaka wa Turin mnamo tarehe 16 Julai akidai alikuwa mlengwa wa njama ya ulaghai ya euro 13m (£11.29m).

Mshindi huyo wa Kombe la Dunia akiwa na Ufaransa mwaka 2018, Pogba alihamia Juventus kwa uhamisho wa huru msimu huu baada ya kuondoka Manchester United.

Mathias Pogba pia ni mwanasoka wa kulipwa ambaye amewahi kuichezea Guinea na amevichezea vilabu mbalimbali barani Ulaya vikiwemo vya Crewe, Wrexham, Crawley na Partick Thistle.