KIPAJI

Nyota wa Man City Haaland anyamazisha wakosoaji

Nyota huyo raia wa Norway amewaacha wakosoaji wake vinywa wazi kutokana na umahiri wake ugani.

Muhtasari

•Wengi walidhani ingemchukua Haaland muda kabla ya kuifahamu vyema falsafa ya kocha Pep Guardiola.

•Pia amefunga hat-trick mfululizo katika mechi tatu za ligi ya nyumbani.

Erling Haaland
Erling Haaland
Image: HISANI

Nyota mpya wa Manchester City Erling Haaland kwa sasa ndiye gumzo la Ligi Kuu ya Uingereza.

Mshambulizi huyo raia wa Norway amewaacha wakosoaji wake vinywa wazi kutokana na umahiri wake ugani.

Huenda msimu wake haukuanza vyema kama wengi walivyotarajia alipokosa kutoa kucha katika mchuano wake wa kwanza Uingereza dhidi ya Liverpool mwezi Julai.

Wengi walidhani ingemchukua Haaland muda kabla ya kuifahamu vyema falsafa ya kocha Pep Guardiola.

Alishutumiwa vikali kwa kushindwa kujihusisha kikamilifu katika kipindi cha kwanza cha mechi yao ya Kombe la Ngao dhidi ya Liverpool alipogusa mpira mara nane pekee katika mechi yote.

Mbaya zaidi, wengi walimkejeli alipogonga nguzo ya goli kutoka yadi sita katika dakika ya mwisho ya mechi kiasi kwamba Guardiola alilazimika kujitokeza kumtetea.

"Ni vizuri kwake kuona ukweli katika nchi mpya na ligi mpya, lakini alikuwepo Hakufunga bao. Ana ubora wa ajabu na atafanya hivyo,” alisema meneja wa City.

Utabiri wa mkufunzi ulijiri siku kadhaa baadaye wakati Haaland alipotulia na kufunga mabao mawili dhidi ya West Ham katika mechi ya kwanza ya City msimu huu.

Kisha alifunga mabao saba katika michezo yake minne iliyofuata, na kuvunja rekodi iliyoshirikiwa hapo awali na Sergio Agüero na Micky Quinn ya mabao mengi zaidi yaliyofungwa katika michezo mitano ya kwanza ya mchezaji kwenye shindano hilo.

Mabao matatu dhidi ya Manchester United siku ya Jumapili yanamaanisha kwamba Haaland amefunga 14 katika mechi zake nane za kwanza za Premier League.

Pia amefunga hat-trick mfululizo katika mechi tatu za ligi ya nyumbani.

Haaland sasa ana wastani wa mabao 1.75 kwa kila mechi na kuna uwezekano wa kufunga zaidi ya mabao 60 msimu huu akiendelea na kiwango hicho.