Aston Villa yampiga kalamu Steven Gerrard baada ya msururu wa matokeo duni

Msemaji wa klabu alisema: "Tungependa kumshukuru Steven kwa bidii na kujitolea kwake na tunamtakia heri kwa siku zijazo."

Muhtasari

• Gerrard alimrithi Dean Smith kama meneja wa Villa mwezi Novemba 2021 baada ya kuacha jukumu lake katika timu ya Rangers.

Aliyekuwa Meneja wa Aston Villa Steven Gerrard
Aliyekuwa Meneja wa Aston Villa Steven Gerrard
Image: GETTY IMAGES

Aston Villa imemfuta kazi meneja Steven Gerrard kufuatia kichapo cha 3-0 cha Ligi ya Premia Alhamisi dhidi ya Fulham.

Msemaji wa klabu alisema: "Tungependa kumshukuru Steven kwa bidii na kujitolea kwake na tunamtakia heri kwa siku zijazo."

Villa wameshinda mara mbili pekee kwenye ligi msimu huu na wamesalia katika eneo hatari la kushushwa daraja kwa mabao ya kufunga.

Gerrard alimrithi Dean Smith kama meneja wa Villa mwezi Novemba 2021 baada ya kuacha jukumu lake katika timu ya Rangers.

Kiungo huyo wa zamani wa England na Liverpool, 42, aliiongoza Villa kushinda jumla ya mechi 13 pekee kati ya mechi 40 katika kipindi cha miezi 11 ya uongozi wake.

Baada ya kushindwa na Fulham, Gerrard alisema : "Kutokuwa na msimamo kumetugharimu, hapo ndipo tunajikuta. Nilichukua timu katika hali kama hiyo. Tumejaribu kusajili ilimkuondoa timu katika hali hiyo.”

Kabla ya kuondoka kwa Gerrard kufichuliwa, nahodha John McGinn alisema:

"Haijalishi ni nani anayesimamia timu hiyo. Haihusiani na meneja - wachezaji wanapaswa kujitazama kwenye kioo. Hakika hatujapoteza imani na [meneja] - ni sisi ambao tunawajibika...

Yeye ni meneja wa hadhi ya juu, anaumia sawia na wachezaji wanavyoumia. Tumemwangusha usiku wa leo. Ni juu yetu sasa kuonyesha kiwango chake."

Gerrard akiwa Villa alisajili wachezaji mashuhuri akiwemo aliyekuwa nyota wa Bracelona Phillipe Coutinho, mlinzi wa Sevilla Diego Carlos na kiungo wa kati Mfaransa Boubacar Kamara, ambaye alikuwa akihusishwa na baadhi ya timu kuu za Ulaya.