Maguire achezeshwa kama mshambulizi dhidi ya Sociedad, azua hatari kwenye goli

Katika zaidi ya dakika 10 ambazo Maguire alikuwa uwanjani kama mshambulizi, alileta mipira mikali ambayo hata hivyo haikufanikiwa kutua nyavuni.

Muhtasari

• Kocha alimtoa mshambuiaji kinda huyo pamoja na kiungo wa kati Eriksen na nafasi zao kuchukuliwa na Maguire pamoja na Fred mtawalia.

Maguire akiwania mpira wa juu dhidi ya mlinzi wa Sociedad
Maguire akiwania mpira wa juu dhidi ya mlinzi wa Sociedad
Image: Getty Images

Kwa wapenzi wa soka watakuambia usiku wa Alhamisi aghalabu huwa ni wa kipekee kwa mechi ya ligi ya Uropa, mashindano ya pili kwa ukubwa baada ya yale ya mashindano ya klabu bingwa Ulaya.

Alhamisi hii timu ya Machester United ilisafiri ugenini kuchuana na Real Sociedad huko Uhispania, katika mechi ya ligi ya Uropa.

Mechi hiyo ambayo United walishinda bao moja komboa ufe ilikuwa na mihemko ya aina yake huku timu hiyo ikiwa uwanjani bila mshambuliaji wa kutegemewa kutokana na wachezaji wake wengi wa safu ya kusaka mabao walikuwa nje kwa majeraha.

Video imesambazwa ikionesha nahodha wa timu hiyo Harry Maguire akicheza kama mshambuliaji mbadala huku akizua mshikemshike karibu na lango lakini kwa bahati mbaya hakufanikiwa kufunga bao hilo alilolisaka kwa udi na ambari.

Mashetani Wekundu walihitaji kushinda mabao mawili ili kuhakikisha wanavuka kama washindi wa kundi, lakini waliambulia patupu, na kushinda bao 1-0 pekee na kulazimika kujiweka sawa katika hatua ya mtoano, itakayochezwa baada ya kukamilika kwa mashindano ya kombe la dunia yatakayong’oa nanga Qatar kuanzia Novemba 20.

Mshambuliaji kinda wa United Alejandro Gernacho alifunga bao hilo la pekee kunako dakika ya 17 ila kocha akaona ukame wa mabao na kuamua kuchukua uamuzi uliwashangaza wengi.

Alimtoa mshambuiaji kinda huyo pamoja na kiungo wa kati Eriksen na nafasi zao kuchukuliwa na Maguire pamoja na Fred mtawalia.

Kwa maana hiyo, Maguire ambaye ni mlinzi wa kati alilazimika kucheza nafasi ya mshambuliaji wa kutegemewa kwa zaidi ya dakika 10 uwanjani kabla mchezo kukamilika.

Majarida yaliripoti kwamba kocha Eric Ten Hag alipoulizwa ni kwa nini alimweka Maguire katika safu ya kutafuta mabao, alisema kuwa ndilo jawabu pekee alilobakia nalo na kuwa alitaka washirikiane na Ronaldo kwani ni miongoni wa wachezaji warefu ambao vichwa vyao vingetegemewa sana kuwahi mipira ya juu.

“Tulihitaji bao na kisha tukaenda kwa nafasi zaidi. Ukiwa na Cristiano na Harry Maguire, una vichwa vizuri vya kuwahi mipira ya juu na tulijaribu kwenda moja kwa moja kwenye eneo la hatari na nadhani tulifanya hivyo mara kadhaa, haraka sana kuingia kwenye boksi kwa mpinzani,” Ten Hag alitetea uamuzi wake.