Hatua kuchukuliwa baada ya shabiki wa Tottenham kumpiga teke kipa wa Arsenal, Ramsdale (+video)

Wasimamizi walijibu haraka na kumzuia shabiki huyo kabla hajampiga tena Ramsdale.

Muhtasari

 •FA imekashifu tabia ya shabiki huyo na kufichua kuwa inashirikiana na polisi na mamlaka nyingine husika kabla ya kuchukua hatua stahiki.

•Mashabiki wa kandanda hasa wafuasi wa Arsenal pia wameendelea kukosoa tukio hilo na kuomba hatua kali zichukuliwe.

alimpiga teke mlinda lango wa Arsenal Aaron Ramsdale baada ya London Derby.
Shabiki wa Tottenham aliyejawa na hasira alimpiga teke mlinda lango wa Arsenal Aaron Ramsdale baada ya London Derby.
Image: HISANI// SKY SPORT

Bodi ya kusimamia soka nchini Uingereza, FA itachukua hatua kufuatia tukio ambapo shabiki mmoja wa Tottenham Hotspur alimgonga teke kipa wa Arsenal Aaron Ramsdale baada ya London Derby iliyochezwa Jumapili jioni.

Siku ya Jumapili, vijana wa Antonio Conte waliwakaribisha majirani wao Wanabunduki ugani Tottenham Stadium. Ziara hiyo hata hivyo iliwaacha wachezaji na mashabiki wa nyumbani wakiwa wamejawa na machungu huku Arsenal ambayo imeendelea kuongoza jedwali ikichukua pointi zote tatu baada ya kushinda 0-2.

Baada ya mchuano huo mkali, kipa Ramsdale alielekea ukingoni mwa uwanja karibu na stendi ili kuchukua glavu zake. Ilikuwa baada ya kuokota glavu zake kutoka chini ambapo shabiki mmoja wa Spurs alimpiga teke kutoka nyuma.

Wasimamizi kadhaa walijibu haraka na kumzuia shabiki huyo aliyejawa na hasira kabla hajampiga tena namba 1 huyo wa Arsenal.

FA imekashifu tabia ya shabiki huyo na kufichua kuwa inashirikiana na polisi na mamlaka nyingine husika kabla ya kuchukua hatua stahiki.

"Hii ni tabia isiyokubalika kabisa na tutashirikiana na polisi, mamlaka husika na vilabu kuhakikisha kuwa hatua zinazofaa zinachukuliwa," msemaji wa FA alisema katika taarifa  siku ya Jumapili jioni.

Mashabiki wa kandanda hasa wafuasi wa Arsenal pia wameendelea kukosoa tukio hilo na kuomba hatua kali zichukuliwe.