Wigan yamfuta kazi Kolo Toure miezi 2 tu baada ya kumteua kama kocha

Akiwa mchezaji, Kolo Toure alizichezea timu za Arsenal, ManCity na Liverpool kama beki wa kutegemewa.

Muhtasari

Beki huyo wa zamani wa Arsenal na Manchester City alitia saini mkataba wa miaka mitatu na nusu alipochukua kazi hiyo Novemba 29.

Kolo Toure afutwa kazi na klabu ya Wigan
Kolo Toure afutwa kazi na klabu ya Wigan
Image: Twitter

Klabu ya Wigan inayoshiriki divisheni ya kwanza nchini Uingereza imemfuta kazi aliyekuwa beki wa timu za Arsenal, Manchester City na Liverpool, raia wa Ivory Coast, Kolo Toure.

Toure anaachishwa kazi miezi miwili tu baada ya kuramba mkataba mpya na timu hiyo lakini akashindwa kutimiza malengo ya timu hiyo ambayo imesalia katika nafasi hatari ya kushushwa daraja hata zaidi.

Jarida la Daily Maily liliripoti kuwa Toure alimwaga unga wake baada ya kushindwa kushinda mechi hata moja kati ya mechi tisa ambazo amekuwa uongozini kama kocha wa Wigan Atletic.

Shaun Maloney anatarajiwa kuchukua nafasi ya Kolo Toure kama meneja wa Wigan, kufuatia kutimuliwa kwa Kolo Toure siku ya Alhamisi.

Graham Barrow anatazamiwa kupangwa kama msaidizi wa Maloney wakati wakijaribu kubadilisha hali mbaya ya timu hiyo. Maloney amekuwa hana kazi tangu atimuliwe kama meneja wa Hibernia msimu uliopita.

Beki huyo wa zamani wa Arsenal na Manchester City alitia saini mkataba wa miaka mitatu na nusu alipochukua kazi hiyo Novemba 29, lakini aliambulia pointi mbili pekee katika mechi saba za ligi na pia kushindwa katika Kombe la FA mikononi mwa Luton katika mchezo wa marudio.

Kipigo cha Jumamosi cha 2-0 nyumbani kwa wapinzani wao hao kwenye ligi kiliiacha Wigan mkiani mwa jedwali, pointi nne kutoka nafasi salama.

Kazi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Toure kama meneja kufuatia majukumu ya ukocha akiwa na nchi yake ya Ivory Coast pamoja na Celtic na Leicester.