Mourinho adokeza kuondoka AS Roma baada ya kupoteza fainali ya Europa dhidi ya Sevilla

"Nataka kubaki AS Roma lakini wachezaji wangu wanastahili zaidi, na mimi pia ninastahili zaidi," alisema.

Muhtasari

•Jose Mourinho amedokeza kuwa hatabaki  katika klabu ya AS Roma baada ya mwisho wa msimu wa 2022/23.

•Mourinho alisema ingawa angetamani sana kuendelea kuisimamia AS Roma, hali si sahihi kwake kusalia.

amedokeza kuondoka AS Roma.
Jose Mourinho amedokeza kuondoka AS Roma.
Image: HISANI

Kocha mashuhuri Jose Mourinho amedokeza kuwa hatabaki  katika klabu ya AS Roma baada ya mwisho wa msimu wa 2022/23.

Mourinho huenda aliiongoza klabu hiyo ya Italia kwa mara ya mwisho siku ya Jumatano jioni walipomenyana na Sevilla ya Uhispania  katika fainali ya Ligi ya Europa ambapo walipoteza katika hatua ya mikwaju ya penalti.

Wakati alipoulizwa kuhusu mustakabali wake baada ya mechi hiyo, meneja huyo wa zamani wa Chelsea, Man United na Tottenham alisema atazungumza kuhusu  hatua yake inayofuata baada  likizo ya muda usiojulikana.

"Mustakabali wangu? Nitaenda likizo Jumatatu. Tutazungumza. Niliwaambia wamiliki (wa Roma) kwamba nitawajulisha kwanza endapo nitafungua mazungumzo na klabu nyingine," Mourinho aliwaambia waandishi wa habari.

Mreno huyo mwenye umri wa miaka 60 alisema ingawa angetamani kuendelea kuisimamia AS Roma, hali si sahihi kwake kusalia.

"Nataka kubaki AS Roma lakini wachezaji wangu wanastahili zaidi, na mimi pia ninastahili zaidi," alisema.

Aliongeza, "Nimechoka kuwa meneja, mkuu wa mawasiliano, uso wa klabu kwenda kusema tumeibiwa.. Nataka kubaki lakini kwa masharti sahihi ili kujitolea yangu yote."

Sevilla walitwaa taji lao la saba la Ligi ya Europa baada ya kuwashinda vijana wa Mourinho mjini Budapest, Hungary kwa mikwaju ya penalti mnamo Jumatano jioni. Mechi hiyo ilikuwa imeisha kwa sare ya 1-1 baada ya dakika 90 za kawaida na za ziada na kupelekea mchuano huo katika mikwaju ya penalti.

AS Roma walifunga penalti yao ya kwanza pekee na kuendelea kupoteza mbili zilizofuata huku Sevilla wakifunga penalti zao zote nne za kwanza na kufanikiwa kushinda kombe hilo. Vijana wa Jose Mourinho walikuwa wamefuzu kwa fainali hizo baada ya kuifunga Bayer Leverkusen ya Ujerumani.