Ronaldo avunja rekodi nyingine tena katika soka ya kimataifa

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 38 amevunja rekodi nyingine na ndiye mchezaji aliyecheza mechi nyingi zaidi katika soka la kimataifa.

Muhtasari

• Licha ya mafanikio yake katika soka, Roanldo hajaonyesha dalili za kuacha kucheza sika ya kulipwa hivi karibuni.

• Akizungumza na GOAL, Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 38 alisema kuwa ataendelea kuwakilisha timu hiyo.

Ronaldo atuzwa rekodi ya Guiness World Record.
Ronaldo atuzwa rekodi ya Guiness World Record.
Image: TWITTER/BR FOOTABALL

Cristiano Ronaldo ameweka rekodi mpya ya dunia baada ya kuichezea timu ya taifa ya Ureno mechi 200 za kimataifa.

Mshambulizi huyo maarufu alicheza mechi yake ya 200 akiwa na Ureno Jumanne,katika mechi yao ya kufuzu kwa Euro 2024 dhidi ya Iceland.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 38 amevunja rekodi nyingine na ndiye mchezaji aliyecheza mechi nyingi zaidi katika soka la kimataifa.

Mafanikio ya Cristiano Ronaldo yametambuliwa na Guinness Book of Records. Nahodha huyo wa Ureno alikabidhiwa cheti cha mafanikio yake kabla ya pambano la timu ya taifa ya Ureno dhidi ya Iceland.

Rekodi hii inaongeza orodha ndefu ya mafanikio ya Ronaldo katika soka ya kimataifa. Mshambuliaji huyo wa Al Nassr ndiye mfungaji bora katika soka la kimataifa akiwa na mabao 122 katika michezo 200 hadi sasa.

Licha ya mafanikio yake katika soka, Ronaldo hajaonyesha dalili za kuacha kucheza soka ya kulipwa hivi karibuni.

Akizungumza na GOAL, Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 38 alisema kuwa ataendelea kuwakilisha timu hiyo.

“Nitakaa hapa hadi mimi, rais [wa shirikisho la soka] na kocha tunamini kuwa naweza. Sitawahi kukata tamaa kuja hapa, kwa sababu hii ni ndoto yangu kwa muda kuichezea timu ya taifa. Ninataka kuendelea kucheza, kuwafurahisha familia yangu, marafiki na Wareno.”

Ronaldo aliichezea Ureno kwa mara ya kwanza mwaka wa 2003 akiwa na umri wa miaka 18. Alishinda Mashindano ya Euro mwaka wa 2016 akiwa na timu yake ya taifa na ataweza kushiriki mashindano hayo yatakayochezwa mwaka ujao.