Messi ateuliwa nahodha mpya wa Inter Miami baada ya kufunga bao mechi ya kwanza

Katika mechi yake ya kwanza, Muajentina huyo aliingizwa uwanjani katika dakika ya 53 ya mchezo na mara moja akapewa kitambaa cha unahodha.

Muhtasari

• Messi anachukua unahodha kutoka kwa Mbrazil Gregore, ambaye amekuwa nje ya timu kutokana na jeraha la mguu.

Messi ateuliwa nahodha Inter Miami.
Messi ateuliwa nahodha Inter Miami.
Image: Instagram

Meneja wa Inter Miami Tata Martino ametangaza kuwa Lionel Messi sasa atakuwa nahodha wa kudumu wa klabu ya MLS Inter Miami, jarida la Khel Now limeripoti.

Mshindi huyo wa kombe la Dunia la Argentina alijiunga na timu ya MLS baada ya kuondoka PSG kama mchezaji huru, licha ya klabu ya zamani ya Barcelona na Klabu ya Saudi Al-Hilal kumtaka.

Uhamisho wa nguli huyo wa kandanda kwenda Miami ulikamilika mwezi uliopita, na alicheza mechi yake ya kwanza katika mechi ya Kombe la Ligi dhidi ya Cruz Azul Jumamosi.

Mechi ya kwanza ya Messi ya Inter Miami ilikuwa ya kufana kwani Muajentina huyo aliingizwa uwanjani katika dakika ya 53 ya mchezo na mara moja akapewa kitambaa cha unahodha.

Mchezo ulipoenda hadi dakika za lala salama, Messi aliutumia vyema mpira wa adhabu katika dakika ya 94 na kufunga bao na kushinda mchezo huo kwa timu yake kama anavyofanya mara nyingi.

Mmiliki mwenza wa Inter Miami David Beckham alisema kwamba wakati mpira wa adhabu ulipotolewa, alihisi kwamba hivi ndivyo sakata hiyo ilipaswa kumalizika.

"Hivi ndivyo, ndivyo inavyoisha" alisema Beckham baada ya mchezo alipokuwa akizungumzia mpira wa adhabu wa Messi.

Mechi ya kwanza ya Messi haikunyimwa nyota wengine. Nyuso nyingi zinazotambulika, akiwemo gwiji wa Mpira wa Kikapu Lebron James, gwiji wa Tenisi Serena Williams, mwanahabari Kim Kardashian na mwimbaji-mtunzi wa nyimbo Marc Antony ndio waliokuwepo.

Messi anachukua unahodha kutoka kwa Mbrazil Gregore, ambaye amekuwa nje ya timu kutokana na jeraha la mguu.

Wachezaji wenzake wa zamani wa Barcelona Sergio Busquets na Jordi Alba wote wameungana na Messi huko Florida na mazungumzo na mchezaji mwingine wa zamani wa Barca Luis Suarez yanaendelea.

Zaidi ya hayo, Messi, Busquets na Alba wanafahamiana vyema na meneja Tata Martino kwa kuwa amewasimamia wakati wakiwa na Barcelona.