Tanzania wafuzu AFCON Kenya wakisherehekea ushindi dhidi ya Qatar mchezo wa kirafiki

Hii ilikuwa ni mara ya tatu kwa Tanzania kufuzu katika mashindano ya AFCON wakati wenzao Kenya waliopigwa marufuku mwaka jana wakisherehekea mechi ya kirafiki isiyo na tija yoyote.

Muhtasari

• Kenya ilifungiwa nje ya kushiriki mchezo wa kufuzu AFCON mwaka jana baada ya serikali kuingilia mgogoro uliokuwa unaendelea katika shirikisho la soka FKF.

• Jumla ya timu 24 zitashiriki michuano ya AFCON itakayofanyika nchini Ivory Coast mwanzoni mwa mwaka ujao.

Afcon
Afcon
Image: Facebook

Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars wamejikatia tikiti kwenda mashindano ya AFCON nchini Ivory Coast kwa mara ya tatu katika historia ya taifa hilo.

Taifa Stars walijikatia tikiti baada ya kulazimisha sare ya kutofungana dhidi ya mabingwa wa mwaka 2019 Algeria.

Taifa Stars imemaliza nafasi ya pili katika kundi F ikiwa na alama 8 na Algeria wakiongoza kundi hilo kwa alama 16. Uganda ambao walikuwa kundi moja na Taifa Stars wameshindwa kufuzu baada ya kukosa pointi moja licha ya kuifunga Niger mabao 2-0 na hivyo kuondoka na alama 7. 

Jumla ya timu 24 zitashiriki michuano ya AFCON itakayofanyika nchini Ivory Coast mwanzoni mwa mwaka ujao.

Ghana na Angola nazo zimefanikiwa kusonga mbele baada ya kumaliza nafasi ya kwanza na ya pili katika kundi E.

Wakati hayo yakijiri, majirani Kenya walikuwa wakishiriki mchezo wa kujipima nguvu dhidi ya mwandalizi wa mashindano ya kombe la dunia 2022, Qatar.

Kenya walikosa adabu za mgeni na kuinyuka Qatar mabao mawili kwa moja, bao la ushindi likifungwa kunako dakika za zima taa tulale.

Kenya ilifungiwa nje ya kushiriki mchezo wa kufuzu AFCON mwaka jana baada ya serikali kuingilia mgogoro uliokuwa unaendelea katika shirikisho la soka FKF ambapo rais wa shirikisho hilo Nick Mwendwa alikuwa ametunguliwa na waziri kuteua kamati ya muda kuongoza FKF.

Kwa mujibu wa sheria za bodi inayosimamia soka duniani FIFA, iwapo serikali itaingilia auc kujihusisha kwa njia yoyote katika shughuli za shirikisho la soka kwa nchi yake, taifa hilo litapigwa marufuku kushiriki mechi za kimataifa katika mashindano mbalimbali rasmi.