•Zoe Maguire amejitokeza kumtetea vikali mwanawe kufuatia chuki nyingi ambazo amekuwa akipokea kwa muda mrefu.
•Mamake Maguire alibainisha kuwa hakufurahishwa na chuki ambayo ilikuwa inaelekezwa kwa mwanawe.
Mama ya beki Harry Maguire, Zoe Maguire Wilkinson amejitokeza kumtetea vikali mwanawe kufuatia chuki nyingi ambazo amekuwa akipokea kwa muda mrefu.
Katika taarifa ya siku ya Alhamisi, Bi Maguire aliyalaani vikali mashambulizi dhidi ya beki huyo mwenye umri wa miaka 30 kutoka kwa mashabiki, wadadisi wa soka na vyombo vya habari akiyataja kuwa ya aibu na yasiyokubalika.
Mamake Harry alisema kwamba alihudhuria mechi ya hivi majuzi ya England dhidi ya Scotland ambapo mchezaji huyo alijifunga bao kwa mara nyingine katika kipindi cha pili na akabainisha kuwa hakufurahishwa na chuki ambayo ilikuwa inaelekezwa kwa mwanawe.
"Kama mama, kuona kiwango cha maoni hasi na matusi ambayo mwanangu anapokea kutoka kwa baadhi ya mashabiki, wachambuzi na vyombo vya habari ni fedheha na haikubaliki kabisa kwa matabaka ya aina yoyote, bila kujali mtu anayejitolea sana kwa klabu na nchi. Nilikuwa pale uwanjani kama kawaida, haikubaliki kilichotengenezwa bila chochote," Bi Zoe Maguire alisema.
Mzazi huyo wa Harry alidokeza kuwa si rahisi kwake kuangalia mwanawe anachofanyiwa uwanjani na kubainisha kuwa asingependa yafanyike kwa mtu mwingine yeyote.
"Ninaelewa kuwa katika ulimwengu wa soka kuna kupanda na kushuka, mambo chanya na hasi, lakini kile Harry anapokea kimeenda mbali zaidi ya mpira wa miguu. Kwangu mimi kumuona akipitia yale anayopitia si sawa. Ningechukia kuona wazazi au wachezaji wengine wakipitia haya siku zijazo, haswa wavulana na wasichana wachanga wakivunja safu leo, " alisema.
Hata hivyo, alidokeza kuwa mwanawe ana nguvu ya kiakili akibainisha kuwa hiyo ndiyo sababu pekee inayomfanya astahimili chuki inayoelekezwa kwake.
"Harry ana moyo mkubwa na ni nzuri nzuri kuwa ana nguvu kiakili na anaweza kuishughulikia kwani wengine hawawezi pia. Sitaki unyanyasaji wa aina hii dhidi ya mtu yeyote,” Bi Maguire alisema.
Harry Maguire ambaye kwa sasa anachezea Manchester United alishambuliwa sana uwanjani na mitandaoni mapema wiki hii baada ya kujifunga bao lingine wakati wa mechi ya England dhidi ya Scotland kwenye uwanja wa Hampden Park, jijini Glasgow.
Beki huyo mwenye umri wa miaka 30 aliingizwa uwanjani katika dakika ya 46 ya mchezo na kufunga kipa wake Aaron Ramsdale kama dakika 20 baadaye.