Arsenal wavunja rekodi mbili ambazo Man City imeshikilia muda mrefu kwa kutoka sare ya 0-0

City walikuwa wamefunga katika mechi 47 mfululizo za EPL kwenye Uwanja wa Etihad kabla ya kumenyana na safu ya ulinzi ya Arsenal.

Muhtasari

•Mara ya mwisho kwa mabingwa hao wa EPL 2022/23 kukosa kufunga Etihad ilikuwa Oktoba 2021 walipopokea kichapo cha 0-2 dhidi ya Crystal Palace.

•Mara ya mwisho kwa Wanabunduki kutopokea kichapo katika uwanja wa Etihad ilikuwa Mei 2016 walipotoka sare ya 2-2.

Image: TWITTER// ARSENAL

Timu mbili zinazopigania kombe la EPL 2023/24, Arsenal na Manchester City mnamo siku ya Jumapili zilicheza mechi ya kusisimua katika uwanja wa Etihad iliyoisha kwa sare ya 0-0.

Ilikuwa ni mara ya kwanza ndani ya miezi mingi kwa Man City kushindwa kufunga katika uwanja wa nyumbani. City walikuwa wamefunga katika mechi 47 mfululizo za ligi ya EPL kwenye Uwanja wa Etihad kabla ya kumenyana na safu ya ulinzi ya Arsenal siku ya Jumapili.

Mara ya mwisho kwa mabingwa hao wa EPL 2022/23 kukosa kufunga Etihad ilikuwa Oktoba 2021 walipopokea kichapo cha 0-2 dhidi ya Crystal Palace.

Mechi ya Jumapili ilikuwa muhimu sana kwa timu hizo mbili kwani zote zimedhamiria kusalia kwenye mbio za ubingwa wa mwaka huu ambazo zimeonekana kuwa ngumu sana.

Liverpool ambao pia wako kwenye kinyang'anyiro hicho mapema siku hiyo walipata ushindi wa 2-1 dhidi ya Brighton & Hove Albion na kupanda juu ya jedwali.

Mabao ya Luis Diaz na Mo Salah yaliwaweka vijana wa Jurgen Klopp mbele na kuwafanya wawe katika nafasi bora ya kushinda kombe kwa sasa.

Mikel Arteta pia aliweza kuvunja rekodi nyingine akiwa Arsenal kwa kuepuka kushindwa tena na Man City katika uwanja wa Etihad. Kwa kutoka sare dhidi ya washindi wa EPL 2022/23, Arteta alifanikiwa kuzuia kupata ushindi mwingine kutoka kwao, jambo ambalo hawajafanikiwa kufanya tangu 2016.

Mara ya mwisho kwa Wanabunduki kutopokea kichapo katika uwanja wa Etihad ilikuwa Mei 2016 walipotoka sare ya 2-2.

Liverpool kwa sasa wako kileleni mwa jedwali la EPL 2023/24 wakiwa na pointi 67, Arsenal wanashika nafasi ya pili wakiwa na pointi 65 huku Man City wakikamata nafasi ya tatu wakiwa na pointi 64.