Rooney apendekeza njia ya Rashford kurejesha ubora wake ni kwenda klabu nyingine

Rashford amekuwa butu mbele ya lango msimu huu, katika kile ambacho Rooney alisema taswira kwenye uso wake anapocheza inaonyesha kabisa kwamba hana furaha kwenye jezi ya Manchester United.

Muhtasari

• Hata hivyo, Rooney alisema kwamba ombi lake ni kumuona Rashford akipata fomu na furaha yake ndani ya Old Trafford.

Rashford
Rashford
Image: X

Gwiji wa Manchester United, Wayne Rooney ameonekana kumshauri mshambuliaji wa sasa wa klabu hiyo Marcus Rashford kuondoka na kwenda klabu nyingine ikiwa anataka kurejesha ubora wake mbele ya lango.

Akizungumza wakati wa mpambano wa Manchester United na Liverpool wikendi iliyopita kwa mujibu wa Manchester Evening News, Rooney alisema kwamba Rashford ni kijana wa Manchester lakini wakati mwingine anashangaa ikiwa kwenda klabu nyingine ndiko kutakuwa mwamko mpya kwa taaluma yake ya ufungaji mabao.

Rashford amekuwa butu mbele ya lango msimu huu, katika kile ambacho Rooney alisema taswira kwenye uso wake anapocheza inaonyesha kabisa kwamba hana furaha kwenye jezi ya Manchester United.

“Sote tunajua ana uwezo na ana sifa zote za kuwa mchezaji wa kiwango cha juu duniani, hilo ndilo jambo la kukatisha tamaa,” mchezaji huyo anayeshikilia rekodi ya mabao mengi kwa Man Utd alisema.

“Msimu uliopita, alienda na kufunga mabao mengi. Lakini msimu huu, hajaanza vyema. Haonekani kuwa na furaha wakati anacheza. Unajiuliza, je, chaguo lake bora ni kuondoka kwenye klabu na kuanza upya? Lakini ni kijana wa Manchester.”

Kwa mujibu wa tetesi za uhamisho wa soka kwenye jarida la Mirror UK, Rashford mwenye umri wa miaka 26, ambaye ana kandarasi hadi 2028, anavutiwa na Paris Saint-Germain, ambayo inatafuta kuchukua nafasi ya Kylian Mbappe.

Hata hivyo, Rooney alisema kwamba ombi lake ni kumuona Rashford akipata fomu na furaha yake ndani ya Old Trafford.

"Ningependa kumuona akirudisha maisha yake ya soka kwenye klabu, akiendelea kufunga mabao na kujaribu kusaidia klabu kushinda mataji. Lakini hakika amekuwa na msimu mgumu,” aliongeza.