Chelsea wakejeliwa kwa kukwepa kutaja jina la Kai Havertz baada ya kufunga mabao dhidi yao

Mashabiki wa Chelsea pia wameonyesha hasira zao dhidi ya Havertz kwa kusherehekea baada ya kuwafunga.

Muhtasari

•Hatua hii ya msimamizi wa mtandao wa kijamii wa Chelsea imekaribisha kejeli nyingi kutoka kwa mashabiki wa soka.

•Mashabiki wa Arsenal hata hivyo wameonyesha sapoti yao kwa mchezaji wao na kumshukuru kwa kuwasaidia na ushindi huo.

Image: TWITTER//

Kiungo mahiri wa Arsenal, Kai Havertz alifunga mabao mawili mazuri dhidi ya klabu yake ya zamani Chelsea wakati wa mechi yao Jumanne usiku.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ujerumani alifunga bao la tatu na la nne la Wanabunduki katika muda wa dakika saba pekee na kuipa klabu yake hiyo mpya ushindi mkubwa wa mabao 5-0.

Mabao mawili ya kiungo huyo mwenye umri wa miaka 24 yalizua mijadala mikali kwenye mitandao ya kijamii, hasa kwa sababu ya mambo mawili ambayo mashabiki walibaini.

Jambo la kwanza, mashabiki wa soka kwenye mitandao ya kijamii waligundua haraka kuwa msimamizi wa akaunti za mitandao ya kijamii  za Chelsea alikwepa kimakusudi kutaja jina la mchezaji huyo wao wa zamani baada ya kufunga mabao dhidi yao. Ilikuwa tu kwa bao la tatu na la nne la Arsenal ambapo msimamizi wa mtandao wa kijamii  wa Chelsea hakutaja jina la mfungaji, ambayo yote yalifungwa na Havertz.

Hatua hii ya msimamizi wa mtandao wa kijamii wa Chelsea imekaribisha kejeli nyingi kutoka kwa mashabiki wa soka kwenye majukwaa mbalimbali ya kijamii.

Jambo la pili, mashabiki wa Chelsea pia wameonyesha hasira zao dhidi ya Kai Havertz kwa kusherehekea baada ya kuwafunga kwenye mechi hiyo ya kusisimua.

Mashabiki kadhaa wa klabu hiyo ya London wamekusanyika katika kurasa za mitandao ya kijamii za mchezaji huyo wa Ujerumani kumkosoa kwa kusherehekea.

Mashabiki wa Arsenal hata hivyo wameonyesha sapoti yao kwa mchezaji wao na kumshukuru kwa kuwasaidia na ushindi huo.

Tazama maoni kutoka kwa baadhi ya watumiaji wa Twitter kuhusu Kai Havertz:

Onsase: Ulisherehekea dhidi ya timu yako ya zamani? Naomba ulie mwisho wa msimu bila taji.

Mel: Nimefurahi sana kwa ajili yako!! Endelea kufaulu na kuzuia kelele mbaya Kai!! Tunakupigia debe.

@cfcbarny: Wewe ni aibu ya mwanasoka, kamwe usishangilie dhidi ya klabu iliyokutengeneza.

@Nino12x: Wewe ni mchezaji asiye na kitu, kwa hivyo uliona tu bora ukachagua kusherehekea. Sikutakii chochote ila mabaya zaidi.

BUKOLA: Unatikisa dunia yangu, sijali mpenzi wangu.