Kompany amezewa mate na Bayern licha ya kushindwa kusaidia Burnley kusalia kwenye ligi

Bayern wamekuwa na gundu la kupata kocha mzuri baada ya makocha kadhaa kukataa kuhusishwa na klabu hiyo katika siku za hivi karibuni, kila kocha wanayejaribu kumtongoza akiwakataa katakata.

Muhtasari

• Bayern walimaliza katika nafasi ya 3 kwenye msimamo wa ligi ya Bundesliga na Tuchel akaweka wazi kwamba anaondoka.

Vincent Kompany
Vincent Kompany
Image: Hisani

Miamba wa Ujerumani Bayern Munich wameripotiwa kumpigia simu kocha wa Burnley, Mbelgiji Vincent Kompany kwa lengo la kumteua kama kocha wao mpya.

Hii ni baada ya Bayern Munich na kocha wa sasa Thomas Tuchel kuafikiana mapema mwaka huu kuvunja mkataba wa Mjerumani huyo ambaye alishindwa kuisaidia Bayern kutetea ubingwa wa Bundesliga kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 12.

Bayern walimaliza katika nafasi ya 3 kwenye msimamo wa ligi ya Bundesliga na Tuchel akaweka wazi kwamba anaondoka, huku klabu hiyo sasa ikiangazia macho yake katika huduma za Kompany ambaye alishindwa kuisaidia Burnley kusalia kwenye ligi baada ya kuwasaidia kupanda kwenye ligi ya EPL mwanzoni mwa msimu huu ambao umekamilika wikendi.

Bayern wamekuwa na gundu la kupata kocha mzuri baada ya makocha kadhaa kukataa kuhusishwa na klabu hiyo katika siku za hivi karibuni.

Walikuwa na nia ya kumsajili Xabi Alonso, ambaye alipanga vyema kampeni ya Bayer Leverkusen ya kushinda taji la Bundesliga ambayo pia imewafanya mabingwa hao wa mara ya kwanza wa Ujerumani pia kutopoteza msimu mzima bila kufungwa, lakini Mhispania huyo ameamua kubaki.

Bayern pia walionyesha nia ya kumnunua Oliver Glasner, ambaye amekuwa na matokeo mazuri tangu achukue kibarua cha Crystal Palace mwezi Februari.

Lakini kama vile wanavyomtafuta Alonso, hatua hii haitarajiwi kutimia kwani Glasner na Palace hawatazami kutengana.

Imeripotiwa kuwa Bayern wamekuwa wakijaribu kumfanya Tuchel kurejea katika klabu hiyo licha ya kutangaza mapema msimu huu kwamba ataondoka katika majira ya joto.

Kocha huyo wa zamani wa Chelsea anadaiwa kutaka kurejea Ligi Kuu ya Uingereza baada ya kuiongoza kwa miezi 14 huko Bavaria.