Barcelona yamtimua kocha Xavi

Xavi ameaachishwa kazi baada ya mazungumzo na rais wa klabu,Joan Laporta.

Muhtasari

•Xavi ataiongoza Barcelona kwa mara ya mwisho Jumapili, watakapoikaribisha Sevilla katika mechi yao ya mwisho ya La Liga msimu huu.

•Flick anapigiwa upato na klabu hio ya Uhispania kama kocha mtarajiwa.

Kocha Xavi Hernandez
Image: HISANI

Barcelona imemfuta kazi meneja Xavi huku kocha wa zamani wa Bayern Munich Hansi Flick akitarajiwa kuchukua nafasi yake.

Xavi ataiongoza Barcelona kwa mara ya mwisho Jumapili, watakapoikaribisha Sevilla katika mechi yao ya mwisho ya La Liga msimu huu.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 44, ambaye alikuwa amepewa kandarasi hadi 2025, alifahamishwa juu ya uamuzi wa klabu hiyo wakati wa mkutano na rais wa klabu Joan Laporta na mkurugenzi wa michezo Deco siku ya Ijumaa .

Mwezi mmoja uliopita Xavi alitangaza kugura  klabuni ,ila kiungo  huyo wa zamani wa Uhispania  akashawishiwa kusalia  na rais wa klabu hio,Laporta mnamo Aprili.

Maoni ya hivi majuzi kutoka kwa Xavi, alifunguka kuhusu matatizo ya kifedha ya klabu.Maneno hayo yanasemekana kumkasirisha Laporta.

 "Tunamshukuru Xavi kwa kazi yake kama kocha tangu alipoanza kuinoa 2021...'Klabu hio ilisema.

Klabu hio pia ilisema, "muundo mpya" utathibitishwa katika siku zijazo, na Flick atasimamia. Mkufunzi huyo mwenye umri wa miaka 59 amekuwa nje ya kazi tangu alipofutwa kazi na klabu ya Bayern, mnamo Septemba 2023. Flick, ambaye alichukua nafasi ya Joachim Low kama meneja wa kitaifa mnamo 2021, alikuwa meneja wa kwanza wa Ujerumani kutimuliwa tangu jukumu hilo lilipoanzishwa mnamo 1926, akishinda mechi 12 tu kati ya 25 alizosimamia.

Msimu wa Flick akiwa na Ujerumani ulikuja baada ya kuiongoza Bayern Munich kushinda mataji matatu mwaka 2020, na kushinda Bundesliga, DFB-Pokal na Ligi ya Mabingwa. Mshambulizi wa Barcelona Robert Lewandowski, 35, alicheza chini ya Flick katika Allianz Arena kwa misimu miwili.

Xavi aliisaidia klabu hiyo kunyakua taji la La Liga na Kombe la Uhispania katika msimu wake wa kwanza, na kuirejeshwa kwenye Ligi ya Mabingwa.

MKufunzi huyo ameongoza Barcelona kwa mechi 141  huku akishinda mechi 89.