Lucas Paqueta ashtakiwa kwa kufanya makosa kimakusudi ili kupata kadi na kuathiri soko la kamari

Inadaiwa kwamba alitaka kupokea kadi ili mtu moja au zaidi kufaidika kutokana na kamari.

Muhtasari

•Mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil mwenye umri wa miaka 26 amesemekana kuvunja sheria za E5 na F3 FA zinazohusiana na kamari.

•Mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil anakanusha makosa yoyote lakini Shirikisho la Soka limemfungulia mashtaka.

wa West Ham ameshtakiwa kwa kukiuka kanuni za FA.
Kiungo Lucas Paqueta wa West Ham ameshtakiwa kwa kukiuka kanuni za FA.
Image: HISANI

Kiungo mahiri wa West Ham Lucas Paqueta amejipata taabani baada ya kushtakiwa na Shirikisho la Soka ya Uingereza kuhusiana na madai ya kukiuka sheria mbili za FA.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil mwenye umri wa miaka 26 amesemekana kuvunja sheria za E5 na F3 FA zinazohusiana na kamari.

Inadaiwa kuwa alijaribu kushawishi soko la kamari kwa kufanya makosa kimakusudi ili kupokea kadi kutoka kwa marefa.

"Inadaiwa kuwa alitaka kuathiri moja kwa moja maendeleo, mwenendo, au kipengele kingine chochote cha, au kutokea kwa mechi hizi kwa kutaka kupokea kadi kutoka kwa mwamuzi kwa madhumuni yasiyofaa ya kuathiri soko la kamari ili kupata  mtu moja au zaidi kufaidika kutokana na kamari,” FA ilisema kwenye taarifa.

Paqueta pia ameshtakiwa kwa ukiukaji mara mbili wa Kanuni ya FA ya F3 kuhusiana na madai ya kukosa kutii Sheria ya FA F2, ambayo inahusiana na kutoa taarifa na stakabadhi.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil anakanusha makosa yoyote lakini Shirikisho la Soka limemfungulia mashtaka kuhusiana na mwenendo wake katika mechi dhidi ya Leicester mnamo Novemba 2022, Aston Villa Machi 2023, Leeds Mei 2023 na Bournemouth Agosti mwaka jana.

"Nimeshangaa na kusikitishwa sana kwamba FA wameamua kunifungulia mashtaka. Kwa muda wa miezi tisa, nimeshirikiana na kila hatua ya uchunguzi wao na kutoa taarifa zote ninazoweza. Ninakanusha mashtaka kwa ujumla wake na nitapingana nao kutumia kila pumzi ili kusafisha jina langu. Kwa sababu ya mchakato unaoendelea, sitatoa maoni yoyote zaidi, " Paqueta alisema katika taarifa kwenye mtandao wa kijamii wa X.

Klabu ya soka ya West Ham imeahidi kusimama na mchezaji wao.

"Klabu inakubali kupokea mashtaka ya FA yaliyopokelewa na Lucas Paqueta kwa madai ya uvunjaji wa sheria zao," msemaji alisema.

Aliongeza, "Lucas anakanusha kabisa ukiukaji huo na ataendelea kutetea msimamo wake kwa nguvu. Klabu itaendelea kuwa karibu na kumuunga mkono mchezaji huyo katika kipindi chote na haitatoa maoni yoyote hadi suala hilo litakapokamilika."

Kiungo huyo mahiri amepewa hadi Juni 3, 2024 kutoa majibu kuhusiana na mashtaka yanayomkabili.