Afueni kwa Erik Ten Hag, Thomas Tuchel akijiondoa katika mbio za kumrithi Old Trafford

United wamehusishwa na makocha kadhaa iwapo wataamua kufanya mabadiliko, akiwemo kocha wa zamani wa Chelsea na Tottenham Mauricio Pochettino, Thomas Frank wa Brentford na Graham Potter.

Muhtasari

• Kocha wa Uingereza Gareth Southgate pia amehusishwa pakubwa na kuhudhuria sherehe za miaka 60 ya kuzaliwa kwa Sir Dave Brailsford mapema mwaka huu.

Mholanzi Erik Ten Hag anaweza akavuta pumzi ya ahueni baada ya ripoti mpya kuibuka kwamba Mjerumani Thomas Tuchel amejiondoa katika kinyang’anyiro cha kuchukua nafasi yake ya ukufunzi katika klabu ya Mancheser United, kwa mujibu wa BBC Sport.

Kocha huyo wa zamani wa Bayern Munich na Chelsea alifikiriwa kuwa miongoni mwa majina yanayozingatiwa na United iwapo wangeamua kuchukua nafasi ya Erik ten Hag.

Tathmini ya baada ya msimu bado haijafikia tamati yake na Ten Hag bado hajajua kama atapata msimu wa tatu kuinoa Old Trafford.

Inafahamika kuwa Tuchel amekutana na mmiliki mwenza wa United Sir Jim Ratcliffe nchini Ufaransa.

Hata hivyo, Mjerumani huyo mwenye umri wa miaka 50, ambaye pia amekuwa na klabu za Borussia Dortmund na Paris St-Germain, anataka kupumzika kufuatia kuondoka kwake Bayern mwishoni mwa msimu uliopita na hatarajii kurejea kwenye ukufunzi msimu ujao.

United wamehusishwa na makocha kadhaa iwapo wataamua kufanya mabadiliko, akiwemo kocha wa zamani wa Chelsea na Tottenham Mauricio Pochettino, Thomas Frank wa Brentford na Graham Potter, aliyewahi kuzifunza Brighton na Chelsea.

Kocha wa Uingereza Gareth Southgate pia amehusishwa pakubwa na kuhudhuria sherehe za miaka 60 ya kuzaliwa kwa Sir Dave Brailsford mapema mwaka huu.

Hata hivyo, mechi ya kwanza ya kirafiki ya United ya kujiandaa na msimu mpya ni siku moja baada ya fainali ya Euro 2024 na Southgate ana mkataba na Chama cha Soka hadi mwisho wa mwaka.