Mashabiki wa Valencia wafungwa jela kwa ubaguzi wa rangi dhidi ya Vinicius Jr

Walidaiwa kumbagua Vinicius Jr mnamo Mei 2023 kwenye mechi kati ya Valencia na Real Madrid.

Muhtasari

•Kwenye kesi iliyoamuliwa Jumatatu 10,Juni 2024  mashabiki watatu walipatikana na hatia ya uchochezi wa ubaguzi wa rangi .

•Wakuu wa La Liga walisifu hatua hiyo wakisema ni ya kipekee tangu kuanzishwa kwa ligi hio;

Vinicius Junior
Image: BBC

Mashabiki watatu wamehukumiwa kifungo cha miezi minane jela na kupigwa marufuku kutoka viwanjani kwa miaka miwili kutokana na unyanyasaji wa kibaguzi dhidi ya Vinícius Júnior huko Mestalla mnamo Mei 2023.

Tukio hilo  ambalo lilitokea wakati Real Madrid waliposhindwa 1-0  kwenye ligi ya LaLiga na Valencia ,lilizua taharuki duniani kote, baada ya nyota huyo wa Brazil kutambua mtu mmoja katika umati wa watu ambaye alikuwa akimtukana kwa ubaguzi wa rangi, na kusababisha mchezo huo kusimamishwa.

Vinícius baadaye alikashifu jinsi viongozi wa Uhispania wanavyoshughulikia suala hilo, akisema;

"ubaguzi wa rangi ni jambo la kawaida katika LaLiga."

Kwenye kesi iliyoamuliwa Jumatatu 10,Juni 2024  mashabiki watatu walipatikana na hatia ya uchochezi wa ubaguzi wa rangi .Mashabiki hao walihukumiwa kifungo cha awali cha miezi 12 gerezani.

Hata hivyo,chini ya kifungu cha 173.1 cha kanuni ya jinai ya Uhispania walipunguziwa hadi miezi minane kwa kukubali kushiriki kwenye matendo hayo. Pia walipokea marufuku ya miaka mitatu ya kutoenda uwanja, iliyopunguzwa hadi miaka miwili kwa sababu hiyo hiyo, na watalazimika kulipa gharama.

Wakuu wa La Liga walisifu hatua hiyo wakisema ni ya kipekee tangu kuanzishwa kwa ligi hio;

"Uamuzi huu ni habari njema kuhusu vita dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Uhispania," rais wa LaLiga Javier Tebas alisema.

Aliongeza ,"Inarekebisha makosa aliyoyapata Vinícius Júnior na kutuma ujumbe wazi kwa watu wanaokwenda kwenye uwanja wa mpira kushambulia wachezaji . LaLiga itawatambua, kuwaripoti na kutakuwa na kifungo kwao."

Wakuu wa Real Madrid pia wametoa onyo kali kwa wale wote ambao watajihusisha na ubaguzi wa rangi wakitaja kuwa kutiwa mbaroni kwa mashabiki hao watatu wa Valencia kutawapa funzo wengine wenye tabia kama hio.