Junior Starlets yailaza Valencia kwenye mechi ya kirafiki

Junior Starlets yailaza mabao 4-1 timu ya wanawake ya Valencia kwenye mechi ya kirafiki katika uga wa Ciudad Deportiva del València CF

Muhtasari

•Starlets wanatumia mechi hizo za kirafiki kama mazoezi huku wakichupia jicho kombe la dunia U-17, huku wakifungua udhia na Young Lionesses wa Uingereza.

•Starlets wamebakisha mechi mbili za kirafiki ambapo watacheza na Ureno pamoja na Intercity kabla ya kindumbwendumbwe cha kombe la dunia kuanza rasmi octoba 16.

STARLETS CELEBRATION AFTER SCORING
Image: HISANI

Timu ya kenya ya wanadada wachanga,Junior Starlets ilidhihirisha ubabe wake baada ya kuilaza timu ya wanadada ya Valencia mabao 4-1 katika mechi ya kirafiki.

Mechi hiyo ilitumiwa kama kipimo cha kutia wanasoka hao wasiozidi umri wa miaka 17 kwenye mizani wakati wanasubiria kucheza katika kipute cha kombe la dunia la wachezaji wasiozidi umri wa miaka 17.

Junior Starlets wameweka orodha ya garambe ambazo watajipima nazo ambazo zilianza Jumatano ya tarehe 25 kwa ushindi.

Starlets walipata mabao yao kupitia kwa wachezaji Valerie Nekesa, ambaye alicheka na nyavu mara mbili kunako dakika ya 9 na 26 baada ya kupata mgongeo mzuri kutoka kwa Halima Imbachi.

Kabla ya kipindi cha kwanza kutamatika,Lindey Atieno alitia bao lingine kimyani na kufunga lingine kunako kipinndi cha pili dakika ya 50 na kuweka jumla ya mabao kuwa manne.

Timu hiyo ya Valencia ilipata bao la kufuta machozi kunako dakika ya 88 kupitia mkwaju wa penati.

Elezabeth Ochaka akizungumza baada ya mechi alisema kuwa,"ilikuwa mechi ya kufana sana kwetu haswa baada ya kupata ushindi huku tukitupia jicho kombe la dunia,tunawazia sana kupata ushindi katika mechi zijazo za kirafiki mbili ambazo zimesalia.Lengo letu kubwa ni kufika katika hatua ya nusu fainali katika kipute hicho,na kupata uzoefu wa kutosha".

Starlets watacheza na Ureno mnamo Septemba 27 na kisha kumalizia na timu ya Intercity mwezi huo 30 katika kampeni zao za mechi za kirafiki kabla ya kipute cha kombe la dunia kwa wachezaji hao wasiozidi umri 17.

Kipute hicho kitakuwa kinaandaliwa katika taifa la Dominican Republic kuanzia Okctoba 16-Novemba 3,2024.

Starlets katika mechi za kufuzu kwa kipute hiki,waliipiku timu ya taifa ya Burundi kwa jumla ya mabao 5-1 na kutinga kwa kipute hicho kwa mara ya kwanza kabisa.

Kocha wa timu hiyo Mildred Cheche ana imani kwa wanadada hao huku akiratibiwa kufungua udhia na timu ya taifa ya Uingereza Alhamisi ya tarehe 17, Oktoba.