Beki wa Arsenal Pablo Mari afanyiwa upasuaji baada ya kudungwa visu mgongoni

Watu wengine watano walijeruhiwa katika shambulio hilo huku mmoja wao akiaga dunia

Muhtasari

•Mari ataendelea kulazwa hospitalini kwa siku mbili ama tatu zaidi baada ya kufanyiwa upasuaji wa kurekebisha misuli miwili ya mgongo iliyojeruhiwa.

•Klabu hiyo imedokeza kuwa Mari atapumzika kwa takriban miezi miwili kabla ya kurejea tena kwenye mazoezi.

Beki wa Arsenal na Monza Pablo Mari
Image: Nicolò Campo/LightRocket via Getty Images

Klabu ya soka ya Italia AC Monza imetoa taarifa kuhusu maendeleo ya beki wa kati Pablo Mari baada ya kudungwa kisu Ahamisi jioni.

Mari ambaye anachezea klabu hiyo ya Serie A kwa mkopo kutoka Arsenal alijeruhiwa mgongoni baada ya kushambuliwa ndani ya  jumba la maduka katika jiji la Milan jana jioni. Watu wengine watano pia walijeruhiwa katika shambulio hilo la kutisha huku mmoja wao akiaga dunia.

Monza imesema kuwa mchezaji huyo wa Uhispania ataendelea kulazwa hospitalini kwa siku mbili ama tatu zaidi baada ya kufanyiwa upasuaji wa kurekebisha misuli miwili ya mgongo iliyojeruhiwa.

"Wataalamu wa upasuaji katika Hospitali ya Niguarda jijini Milan walifanya upasuaji wa kujenga upya misuli miwili iliyojeruhiwa kwenye mgongo wa Pablo Marí. Upasuaji ulikwenda vizuri na atakaa hospitalini kwa siku mbili au tatu. Baada ya kutoka, mchezaji huyo ataweza kuanza mchakato wa kurejesha afueni," sehemu ya taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti rasmi ya Monza ilisoma.

Klabu hiyo imedokeza kuwa Mari atapumzika kwa takriban miezi miwili kabla ya kurejea tena kwenye mazoezi.

Alhamisi jioni, Arsenal ilichukua hatua ya kumtakia afueni ya haraka beki huyo kufuatia tishio hilo dhidi ya maisha yake.

"Sote tumeshtushwa kusikia habari mbaya kuhusu tukio la kuchomwa visu nchini Italia, ambalo limewaweka watu kadhaa hospitalini akiwemo beki wetu wa kati anayecheza kwa mkopo Pablo Mari. Tumekuwa tukiwasiliana na ajenti wa Pablo ambaye ametuambia yuko hospitalini na hajaumia sana," Arsenal ilisema katika taarifa.

Klabu hiyo ya London ilituma ujumbe wake wa faraja kwa Pablo na wahasiriwa wengine watano wa tukio hilo la kuogofya.

Shambulizi hilo lilijiri jioni ambapo Wanabunduki walipata kichapo cha aibu dhidi ya PSV  ya Uholanzi katika mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Europa. PSV ilipiga Arsenal 2-0 katika mechi ya mkondo wa pili.