Beki wa kati wa Arsenal na Ufaransa, William Saliba afuatilia asili yake nchini Cameroon

Marehemu mamake Saliba alikuwa Mkameruni ilhali baba yake ni mzaliwa wa Lebanon.

Muhtasari

•Saliba ameonekana akitangamana na wanafamilia wake na wenyeji wa mtaa ambao marehemu mamake alizaliwa.

•Kwa bahati mbaya, Saliba aliwapoteza wazazi wake wote wawili miaka michache iliyopita, babake akitangulia.

akifurahia muda Cameroon.
Saliba akifurahia muda Cameroon.
Image: HISANI

Beki wa kati matata wa Arsenal, William Saliba kwa sasa anafurahia likizo nchini Cameroon.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 23 aliwasili katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi siku chache zilizopita na amekuwa akishiriki muda na familia yake iliyo katika eneo la Douala.

Picha na video zimeibuka kwenye mitandao ya kijamii zikimuonyesha mchezaji huyo mahiri akitangamana na baadhi ya wanafamilia wake na wenyeji wa mtaa ambao marehemu mama yake alizaliwa.

Katika moja ya video ambazo zimekuwa zikisambazwa, mchezaji huyo wa Arsenal anaonekana akiwa amevalia kaptula nyeupe na bluu na tshirt nyeupe huku akiwasalimia baadhi ya wenyeji mjini Douala. Bendi ya vijana pia wanaonekana wakimtumbuiza kwa muziki na densi.

Beki huyo pia alionekana akipigwa picha na baadhi ya wanafamilia.

Haijabainika ni muda gani atakaa katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi lakini anatarajiwa kurejea nchini Ufaransa hivi karibuni kujiunga na kambi ya mazoezi ya timu ya taifa kabla ya michuano ya Euro 2024 itakayoanza katikati mwa mwezi Juni.

Takriban mwaka moja uliopita, Saliba alionekana tena nchini Cameroon akifurahia muda na baadhi ya wanafamilia na mashabiki wake.

Pia alikutana na nyota wa zamani wa soka  wa nchi hiyo Samuel Eto’o ambaye alishiriki muda naye na hata kutazama mechi ya soka naye katika moja ya viwanja nchini Cameroon. Eto'o , 42, kwa sasa ndiye rais wa Shirikisho la Soka la Cameroon kuanzia tarehe Desemba 2021 kufuatia kustaafu mwaka 2019.

Mchezaji huyo mahiri wa timu ya taifa ya Ufaransa aliamua kutumia likizo yake ya jeraha kuwatembelea wanafamilia wake nchini Cameroon. Marehemu mama yake anaamikia kutoka nchi hiyo ya Afrika Magharibi ilhali baba yake, Brian Robertson alitoka nchi ya  Lebanon, barani Asia.

Kwa bahati mbaya, Saliba aliwapoteza wazazi wake wote wawili miaka michache iliyopita, babake akitangulia.