Chelsea yamtimua Kocha Mkuu Thomas Tuchel

Tuchel alipigwa karamu masaa machache tu baada ya kupoteza 1-0 kwa Dinamo Zagreb.

Muhtasari

•The Blues walitangaza habari za kutimuliwa kwa Tuchel Jumatano adhuhuri kupitia tovuti rasmi ya klabu.

•Uamuzi wa kumtimua kocha huyo ulifanywa na kundi jipya la umiliki katika juhudi za kuisukuma klabu mbele.

Aliyekuwa Kocha wa Chelsea Thomas Tuchel
Image: CHELSEA.COM

Klabu ya Chelsea imempiga kalamu kocha wao  mkuu Thomas Tuchel.

The Blues walitangaza habari za kutimuliwa kwa Tuchel Jumatano adhuhuri kupitia tovuti rasmi ya klabu.

"Klabu ya soka ya Chelsea leo imeachana na Kocha Mkuu Thomas Tuchel," taarifa iliyotolewa na Chelsea ilisoma.

Katika taarifa yake, Chelsea ilitoa shukrani kwa Mjerumani huyo pamoja na timu yake ya ukufunzi ambayo pia imeonyeshwa mlango.

"Thomas atakuwa na nafasi katika historia ya Chelsea baada ya kushinda Ligi ya Mabingwa, Kombe la Super Cup na Kombe la Dunia la Klabu katika wakati wake hapa," taarifa hiyo ilisoma.

The Blues  walidokeza kuwa uamuzi wa kumtimua kocha huyo ulifanywa na kundi jipya la umiliki katika juhudi za kuisukuma klabu mbele.

Kulingana na taarifa iliyotolewa, kundi la umiliki wa klabu hiyo lilionelea  ni sawa kufanya mabadiliko hayo kwa wakati huu.

"Wakufunzi wa Chelsea watasimamia timu kwa mazoezi na maandalizi ya mechi zetu zijazo huku Klabu ikipiga hatua kwa haraka kuteua kocha mkuu mpya,

Tuchel alifutwa na klabu hiyo masaa machache tu baada ya kupoteza 1-0 kwa Dinamo Zagreb katika mechi yao ya kwanza ya Champions League msimu huu.

Jumanne usiku The Blues walipoteza mechi yao ya kwanza kwenye Kundi E  kufuatia bao la pekee la Mislav Orsic katika dakika ya 13.

Kwenye EPL Chelsea kwa sasa wameshikilia nafasi ya sita baada ya kupoteza mechi mbili na kuandikisha sare moja katika mechi tano za kwanza.