Haachi! Mshambulizi Erling Halaand avunja rekodi nyingine kubwa ya Ligi Kuu Uingereza

Halaand amevunja rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi katika msimu mmoja wa EPL katika msimu wake wa kwanza.

Muhtasari

•Erling Halaand alifunga bao la pili la Man City wakati wa ushindi muhimu wa 3-0 dhidi ya klabu ya West Ham.

•Ushindi wa Jumatano usiku uliwaweka Man City katika nafasi bora ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara nyingine.

Mshambulizi Erling Halaand
Image: HISANI

Mshambulizi wa Manchester City Erling Haaland alivunja rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi katika msimu mmoja wa Ligi Kuu ya Uingereza siku ya Jumatano usiku baada ya kufunga bao lake la 35 wakati wa mechi dhidi ya West Ham United.

Halaand alifunga bao la pili la Man City wakati wa ushindi muhimu wa 3-0 dhidi ya wapinzani wao kutoka London kwenye Uwanja wa Etihad na kuwafanya mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza kurejea kileleni mwa jedwali la EPL.

Bao la kwanza la klabu hiyo inayosimamiwa na Pep Guardiola lilifungwa na beki Nathan Ake katika dakika ya 50 huku mshambulizi Phil Foden ambaye aliingia uwanjani katika kipindi cha pili akifunga bao la ushindi katika dakika ya 85.

Kwa miaka mingi, mchezaji wa zamani wa Newcastle United, Alan Shearer alikuwa akishikilia rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi ya Ligi Kuu ya Uingereza ndani ya msimu mmoja, akiwa na mabao 34, pamoja na staa wa zamani wa Manchester United Andy Cole. Lakini bao lililofungwa na Erling Haaland katika kipindi cha pili dhidi ya West Ham lilimfanya apite mbele ya wawili hao na kusajili mabao 35 katika msimu wa Ligi Kuu ya Uingereza - na bado kuna michuano mitano iliyosalia kuongeza jumla ya mabao yake.

Ushindi wa Jumatano usiku uliwaweka Man City katika nafasi bora ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara nyingine.

Vijana wa Pep Guardiola, ambao wanawinda taji la tano katika misimu sita chini ya mkufunzi huyo, wana pointi 79 kutoka kwa michuano 33 huku Arsenal wakiwa na pointi 78, wakiwa wamecheza mechi moja zaidi. Watasonga mbele kwa pointi nne ikiwa watashinda Leeds United nyumbani Jumamosi.