"Heri ningekaa!" Lejendari wa Arsenal ajutia sana kuondoka klabu hiyo juu ya mwanamke

Petit alikiri kwamba aliondoka Arsenal kwa sababu ya mwanamke, uamuzi ambao sasa anajutia.

Muhtasari

•Petit amefunguka kuhusu uamuzi wake wa kuondoka katika Klabu ya Arsenal ili kujiunga na Barcelona zaidi ya miongo miwili iliyopita.

•Petit alikiri anajutia sana uamuzi wake wa kuhama akisema kwamba ikiwa saa ingerudishwa, basi angechukua chaguo tofauti

Aliyekuwa mchezaji wa Arsenal, Emmanuel Petit
Image: HISANI

Mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa, Emmanuel Petit amefunguka kuhusu uamuzi wake wa kuondoka katika Klabu ya Arsenal ili kujiunga na Barcelona zaidi ya miongo miwili iliyopita.

Petit aliondoka Arsenal na kujiunga na klabu hiyo ya Laliga mwaka wa 2000 lakini alikaa Nou Camp kwa msimu mmoja tu kabla ya kurejea Uingereza kuichezea Chelsea.

Katika mahojiano ya hivi majuzi na The Express, mwanasoka huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 53 alikiri kwamba aliondoka Arsenal kwa sababu ya mwanamke, uamuzi ambao sasa anajutia.

"Ilikuwa kwa sababu ya mwanamke, ndio," Petit alisema.

Kiungo huyo wa kati wa zamaniu alikubali kuwa mwanamke aliyekuwa akichumbiana naye alitaka kuhama kutoka Uingereza na hilo lilimfanya ahamie Uhispania.

"Siku zote nilipenda Barcelona na [Real] Madrid, ni sehemu ya vilabu vikubwa zaidi duniani. Lakini nilipaswa kubaki na Arsenal, bila shaka," alisema huku akitikisa kichwa.

Aliongeza, “Unajua wakati fulani nyasi si nzuri zaidi mahali pengine. Ni bora kukaa hapo ulipo. Unapopokea upendo na furaha, na ukafanikiwa, kwa nini unaondoka?"

Petit alikiri kwamba anajutia sana uamuzi wake wa kuhama akisema kwamba ikiwa saa ingerudishwa, basi angechukua chaguo tofauti.

Uamuzi wa mchezaji huyo kuondoka Arsenal haukuwafurahisha mashabiki wa klabu hiyo ya London kwani tayari alikuwa akipata upendo mwingi alipokuwa akiichezea.

Uhusiano wake na mashabiki uliendelea kuwa mbaya zaidi wakati alipohamia kwa wapinzani wao wakubwa, Chelsea, baada ya mwaka mmoja tu Barcelona.

Kiungo huyo wa kati alikaa kwa misimu mitatu katika Stamford Bridge kabla ya kustaafu kutokana na matatizo yaliyotokana na upasuaji wa goti.